BARABARA ZENYE VIWANGO KUPANDISHWA HADHI KWENDA TANROADS" OR-TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amesema TARURA kwa kushirikiana na Bodi ya Barabara ya Mkoa itaanzisha mchakato wa kuzipandisha hadhi barabara hizo katika mwaka 2025/26 ili ziweze kuwa chini ya TANROADS.
Mhe. Katimba ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe. Masache Njeru Kasaka aliyetaka kujua "Je, lini Serikali itazipandisha hadhi barabara ya Isenyela - Sangambi - Lupa - Lualaje na Chunya Godima - Sangambi kuwa chini ya TANROADS.?”
“Suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa. Ikiwa kuna barabara ambayo inakidhi vigezo kutoka daraja la barabara ya wilaya kwenda daraja la barabara ya mkoa inatakiwa barabara hiyo ijadiliwe kwenye kikao cha Bodi ya barabara ya Mkoa husika na ikionekana inakidhi vigezo” amesema
Amesema bodi hiyo kupitia mwenyekiti itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo vya kuwa na hadhi ya barabara ya Mkoa na hivyo ipandishwe daraja na kuwa barabara ya Mkoa chini ya TANROADS.




