Breaking News

BALOZI MATINYI AKUTANA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SWEDEN

Stockholm, Sweden – Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Mhe. Maria Malmer Stenergard, katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Stockholm.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Matinyi aliwasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi na Serikali ya Ufalme wa Sweden. Aidha, alisisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Balozi Matinyi alieleza kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha uchumi wake kupitia ushirikiano na Sweden katika sekta za nishati, elimu, afya, utafiti, mazingira, viwanda na miundombinu, ikiwemo mradi wa Reli ya Kisasa (SGR). Alibainisha pia kuwa hadi sasa jumla ya kampuni 101 kutoka Sweden zimewekeza Tanzania kwa thamani ya dola za Marekani milioni 313.04 na kutoa ajira kwa takribani watu 3,877.

Kwa upande wake, Waziri Stenergard alithibitisha dhamira ya Sweden kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta za biashara na uwekezaji. Pia alisisitiza mchango muhimu wa Tanzania katika kudumisha amani na usalama duniani, hususan katika juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Ukraine na Urusi.