Breaking News

MWIRU AHITIMISHA KAMPENI DAR: AAHIDI SERIKALI YA MCHAKAMCHAKA YENYE NIDHAMU NA UZALENDO

Dar es salaam - Mgombea urais kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, amehitimisha kampeni zake jijini Dar es Salaam, akiahidi kuunda Serikali ya mchakamchaka yenye miaka mitano endapo ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 17, 2025, katika viwanja vya Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke, Mwiru alisisitiza kuwa Serikali yake haitakimbilia mchakato wa Katiba mpya, badala yake itaitumia Katiba iliyopo kwa heshima ya waasisi wa taifa.

“Mimi lazima niwaenzi wazee wangu walioandaa Katiba hii. Nikiwa Rais, nitaanzisha madarasa ya kuwafundisha wananchi kuhusu Katiba. Mtanzania apewe fursa ya kusoma Katiba mbili – ya zamani na ya sasa – ili aamue ipi inamfaa,” alisema.

Kipaumbele kwa Huduma za Jamii

Mwiru aligusia changamoto za sekta ya afya, akiahidi kujenga nyumba za watumishi wa zahanati ndani ya mwaka mmoja ili kurahisisha utoaji wa huduma. Pia aliahidi kuboresha maslahi ya walimu na askari polisi, akiwataja kama nguzo muhimu za taifa zinazofanya kazi katika mazingira magumu.

Mapambano Dhidi ya Ufisadi

Mgombea huyo alitangaza mpango wa kuunda Task Force ya kufuatilia miradi ya umma, huku akiahidi adhabu kali kwa mafisadi, ikiwemo kuwapeleka “kwa mamba Ikulu.”

Uchumi na Kodi

Mwiru alisema Serikali yake itapunguza makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara wadogo, lakini itahakikisha makusanyo yanaboreshwa. Alionya wadaiwa sugu wa kodi kuwa hawatavumiliwa.

Masuala ya Jamii na Maadili

Akizungumzia changamoto za kijamii, Mwiru aliahidi:

Kuwazuia madaktari kuzuia maiti kwa familia zisizo na uwezo, akisema maiti zitachukuliwa bure.

Kuweka mfumo wa ukusanyaji taka bila malipo nchi nzima, kila mtaa ukipewa lori maalumu.

Kuunda baraza dogo la mawaziri lisilozidi 15 ili kubana matumizi.

Kuwezesha waandishi wa habari kushirikiana na Ikulu kupitia taarifa za vijijini.

Aidha, alikemea tabia za kigeni anazodai “zinapotosha maadili ya Kitanzania,” akisisitiza kuwa wanamuziki wa kiume watakaovaa hereni watapigwa viboko 12 Ikulu.

Mwiru pia aliahidi kujenga madarasa kila kata kwa ajili ya kufundisha uzalendo na maadili, akiwatumia wastaafu wenye afya njema, na kupiga marufuku viongozi wa dini kuingia kwenye siasa.

Aidha ameitimisha kwa kusema kuwa SERIKALI yake itamuwa ni ndogo, yenye nidhamu, inayopambana na ufisadi, na yenye msisitizo mkubwa katika uzalendo na maadili ya Kitanzania.