POLISI YAWATAHADHARISHA VIJANA JUU YA MIPANGO YA VURUGU YA MAANDAMANO
Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kali dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu na uharibifu wakitumia kisingizio cha “maandamano ya amani yasiyo na kikomo” yanayodaiwa kuanza tarehe 9 Desemba 2025. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dhamira ya miito hiyo ni kuvuruga amani na kuathiri maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa taatifa yake kwa vyombo vya habari, Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, amesema vyombo vya Ulinzi na Usalama vinafuatilia kwa ukaribu mawasiliano na mipango yote hatarishi inayoenezwa mtandaoni. Amesema Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha ya watu na mali zao, sambamba na kudumisha amani, utulivu na usalama nchini.
Kwa mujibu wa Polisi, baadhi ya makundi mtandaoni yanahamasisha vitendo vya uharibifu ikiwemo kuchoma minara ya mawasiliano ili kuifanya nchi ikose mawasiliano, kufunga Bandari ya Dar es Salaam, na kuzuia mipaka yote ya kuingia na kutoka nchini. Aidha, wahamasishaji wanadaiwa kupanga kuvuruga huduma za hospitali ili kusimamisha shughuli muhimu za kitaifa.
Katika upande wa usalama wa raia, taarifa hiyo inaeleza kuwa vijana wanahamasishwa kupora mali za wananchi na kuwadhuru watumishi wa Serikali. Pia, kuna madai ya maelekezo yanayotolewa kuhusu matumizi ya silaha kwa washiriki wenye mafunzo maalumu.
Jeshi la Polisi limepongeza wananchi na makundi ya vijana wanaopinga miito ya vurugu na waliojitokeza kuunga mkono juhudi za kulinda amani katika maeneo yao. Limewataka vijana kukataa kutumiwa kisiasa na kutanguliza maslahi ya Taifa.
DCP Misime amewatoa hofu wananchi wote wapenda amani, akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara na tayari kuhakikisha hakuna atakayevuruga utulivu wa nchi. Amesema wote watakaojihusisha na uchochezi wa vurugu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, wananchi wamekumbushwa kuendelea na maandalizi ya sherehe za mwisho wa mwaka kwa kuzingatia usalama wa maisha na mali zao, huku wakihimizwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Jeshi la Polisi limetahadharisha kwamba Tanzania itaendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu, na hakuna mwananchi atakayenyanyaswa au kuzuiwa kutekeleza shughuli zake za kila siku.




