BRELA YAENDELEZA MKAKATI WA KUSOGEZA HUDUMA ZAKE KWA WANANCHI, NJOMBE.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeendelea na mkakati wake wa kuwafikia wafanyabiashara kwenye maeneo yao kwa kuwasogezea huduma zote muhimu za urasimishaji biashara, kutoa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa mkoa wa Njombe.
Hatua ya kusogeza huduma za papo kwa papo kwa wananchi inalenga kuwaondolea changamoto za kupata huduma za Usajili wa Kampuni, Majina ya Biashara, Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi A, Utoaji wa vyeti na Leseni za Viwanda, Usajili wa Alama za biashara na Huduma pamoja na Utoaji wa hataza.
Awali akiwakaribisha Maafisa wa BRELA ofisini kwake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe (RAS), Muhandisi. Joseph Rutashubilwa, aliipongeza BRELA na kusema kuwa mkakati huo unawaweka wadau wake karibu zaidi na kwamba ni fursa adhimu kwa wananchi wa mkoa wa Njombe.
Aidha, Muhandisi. Rutashubilwa alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Njombe, hususan Njombe Mjini, Makambako, Ludewa na Makete kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Soko Kuu la Njombe kutumia fursa hiyo ili kupata huduma, kutatua changamoto zao na kurasimisha biashara kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Afisa Msaidizi wa Usajili kutoka BRELA, Bi. Fatma Jumanne, alieleza kuwa uwepo wa BRELA mkoani Njombe ni muendelezo wa mkakati wa Wakala kufanya Kliniki za Biashara nchi nzima inayolenga kutoa huduma zote muhimu za BRELA kwa wakati mmoja pamoja na elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwasilisha taarifa za wamiliki Manufaa.
Vilevile Bi. Fatma alibainisha kuwa elimu inayotelewa katika kliniki hiyo inalenga kuwajengea wananchi uelewa mpana juu ya dhana ya Umiliki wa Manufaa ili kuhakikisha Kampuni zinaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria na zinawaletea thamani halisi katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Uwepo wa BRELA mkoani Njombe kuanzia tarehe 26 hadi 31 Januari, 2026 katika viwanja vya Soko Kuu la Njombe Mjini unatarajiwa kuongeza mwitikio wa wananchi katika kurasimisha biashara zao, kuimarisha mazingira bora ya biashara na kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi katika mkoa huo.




