KAMATI KUU YA ACT WAZALENDO YAJA NA MAAZIMIO SITA KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2025
Dar es Salaam - Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imekutana katika kikao chake cha kawaida jana, Januari 18, 2026, katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo kwenye Jengo la Maalim Seif, Makao Makuu ya chama, jijini Dar es Salaam, na kutoa maazimio mazito kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na mustakabali wa demokrasia nchini.
Akisoma maadhimio hayo Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Rashid Mchinjita amesema Kamati Kuu ilipokea na kujadili kwa kina taarifa ya Uchaguzi Mkuu 2025 kwa pande zote za Muungano, kisha kutoa tathmini na maamuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa, kikatiba na kiusalama.
Uchaguzi Mkuu 2025 wakosa uhalali
Kamati Kuu imesisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 haukuwa huru, wa haki wala wa kuaminika, na kwamba Serikali iliyoundwa haikutokana na ridhaa ya wananchi. Kwa msingi huo, Kamati Kuu imetangaza kuwa uchaguzi huo unapaswa kurudiwa ili kuwarejeshea Watanzania haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Kamati hiyo imeipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa chama kwa kufungua mashauri 84 mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi na kutetea haki ya wananchi, pamoja na kuwapongeza mawakili wa chama wanaoendelea na kesi hizo, ikiwemo shauri la msingi kuhusu uhalali wa matokeo ya ubunge nchi nzima.
Aidha, Kamati Kuu imelaani vikali mgawanyo wa viti maalumu kwa vyama vya siasa, ikieleza kusikitishwa na ACT Wazalendo kunyimwa viti hivyo licha ya kupata kura 2,222,162 sawa na asilimia 6.8 ya kura zote halali za ubunge, na hivyo kuvuka kizingiti cha kikatiba cha asilimia 5. Kamati Kuu imesema ina imani Mahakama itatenda haki.
Alisema matukio ya yaliyoripotiwa siku ya uchaguzi oktoba 29, Kamati Kuu ksa kauli moja imeazimia kuendelea kuyalaani na kuitaka Serikali kuwawajibisha wote waliohusika kupanga na kutekeleza mauaji hayo. Pia imeitaka Serikali kutoa takwimu sahihi za waliopoteza maisha, kukabidhi miili ya marehemu kwa ndugu zao, na kuunda Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi badala ya tume ya ndani inayowajibika kwa Rais.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar
Kamati Kuu imewashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kukipa imani ACT Wazalendo na mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, pamoja na wagombea wengine katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Hata hivyo, Kamati Kuu imesisitiza kuwa msimamo wa chama hauhusu kuingia au kutokuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), bali ni kusimamia haki ya Wazanzibari ya kuchagua na kuchaguliwa. Imeeleza kuwa SUK haikukusudiwa kuwa njia ya kuhalalisha wizi wa kura, na kwamba ACT Wazalendo itaendelea kushiriki katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa kwa lengo la kurejesha haki ya wananchi.
Vyombo vya ulinzi na usalama
Katika azimio lingine, Kamati Kuu imesema mfumo wa kikatiba na michakato ya kisiasa nchini umetekwa na vyombo vya ulinzi na usalama, hali iliyoifanya Tanzania isiwe demokrasia bali “securocracy”. Kamati Kuu imetaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kurejesha siasa mikononi mwa wananchi kupitia vyama vya siasa.
Mchakato wa Katiba Mpya
Kamati Kuu imetangaza kuwa ACT Wazalendo kitaongoza mapambano ya kudai Katiba Mpya, ikisisitiza kuwa bila Katiba Mpya hakuna demokrasia ya kweli. Chama kimependekeza marekebisho ya sheria za mchakato wa katiba na kura ya maoni sambamba na kuitishwa kwa Mkutano wa Kitaifa wa wadau, kuundwa kwa Kamati ya Wataalamu kuandaa rasimu ya katiba, na hatimaye kufanyika kwa kura ya maoni ya kitaifa.
Kumpongeza Jaji Warioba
Kikao hicho cha Kamati Kuu pia imempongeza Jaji Joseph Sinde Warioba kwa ujasiri wake wa kutetea misingi ya haki na utawala wa sheria, na kukitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwakemea viongozi wake wanaomdhalilisha.




