PROF. LIPUMBA AWASIHI WATANZANIA KUKATAA UBAGUZI WA DINI NA KIJIOGFAFIA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amewasihi Watanzania kutokubali kubaguliwa kwa misingi ya dini, siasa, au tofauti za kijiografia kati ya Tanzania Bara (Tanganyika) na Zanzibar.
Prof. Lipumba ametoa wito huo leo Januari 27, 2026, wakati wa dua ya kuwaombea wanachama wa CUF waliopoteza maisha katika maandamano yaliyofanyika Januari 27, 2001, huko Pemba na Unguja, Zanzibar. Dua hiyo imefanyika kuadhimisha miaka 25 tangu kutokea kwa maandamano hayo yaliyofuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2000.
Akizungumza katika tukio hilo, Prof. Lipumba amesema Watanzania hawapaswi kuruhusu ajenda za ubaguzi wa kidini, kisiasa au kikanda kupewa nafasi, akisisitiza kuwa athari za kuyumbishwa kwa amani na mshikamano wa taifa huwagusa wananchi wote.
“Watanzania tusikubali agenda ya kubaguana kwa misingi ya kidini, kisiasa au Utanganyika na Uzanzibari, kwani Tanzania ikiharibika wote tumeharibikiwa,” amesema Prof. Lipumba.
Ameongeza kuwa changamoto zinazojitokeza nchini zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya amani na utulivu, ili kulinda misingi ya haki, amani na mshikamano wa taifa.
Aidha, Prof. Lipumba amepinga madai kwamba matukio yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2001 na 2025 yalitokana na udini, akieleza kuwa chanzo kikuu kilikuwa ni hisia za kukosekana kwa haki, hususan katika kutangazwa kwa washindi ambao, kwa mujibu wake, hawakuchaguliwa na wananchi.
Amesisitiza umuhimu wa haki katika michakato ya kidemokrasia kama msingi wa kudumisha amani na utulivu nchini.




