CUF YAAZIMIA KURUDIWA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA TAIFA, FOMU ZAANZA KOTOLEWA RASMI
Dar es salaam, Februari 20, 2026 – Kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Chama cha Wananchi (CUF) kimeazimia kurudiwa kwa uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi wa chama hicho, ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao kilichofanyika leo katika makao makuu ya chama, Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Akisoma maazimio ya kikao hicho, Katibu wa kikao, Mussa Mbarouk, amesema wajumbe wa Baraza Kuu kwa kauli moja waliridhia kurudiwa kwa uchaguzi huo ili kupata viongozi watakaokidhi matakwa ya Katiba ya chama.
“Katika kikao kilichofanyika mapema leo katika Ukumbi wa Shaabani Mloo, wajumbe wameazimia kwa kauli moja kuwa viongozi waliokuwepo madarakani hawajakidhi matakwa ya Katiba ya chama, hivyo kuamua kurudia uchaguzi kwa ajili ya kupata viongozi wapya,” alisema Mbarouk.
Ameeleza kuwa kufuatia maamuzi hayo, chama kimefungua rasmi kuanzia saa 8 mchana leo, Februari 20, 2026, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa wanachama wanaokidhi vigezo. Nafasi hizo ni pamoja na ile ya Mwenyekiti wa Taifa, ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Ibrahim Lipumba.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa wa chama hicho, Dauda Hassan Kasingwa, amewataka wanachama wa CUF kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Amebainisha kuwa zoezi la kuchukua na kurejesha fomu litaendelea hadi kesho, Februari 21, 2026, saa 3 asubuhi, ambapo litafungwa rasmi na kufuatiwa na uchaguzi utakaofanyika katika Ukumbi wa Lekam, Buguruni.
Chama kimesisitiza kuwa mchakato huo unalenga kuimarisha uongozi na kuhakikisha kuwa viongozi watakaochaguliwa wanazingatia kikamilifu Katiba na misingi ya chama hicho.




