Breaking News

TANZANIA NA UGANDA ZAENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA NA KIUCHUMI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha tano cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission - JPC) kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Bagiire Vincent akifafanua jambo kikao cha tano cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission - JPC) kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa kikao cha tano cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission - JPC) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi, kikao kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.



Dar es salaam - Tanzania na Uganda zimeendelea kuimarisha uhusiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi kupitia kikao cha tano cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission - JPC) kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samweli Shelukindo, amesema uhusiano kati ya nchi hizo mbili umejengwa katika misingi ya maadili ya pamoja, kuheshimiana na kuwa na maono yanayofanana ya maendeleo.

Amesema kwa miaka mingi Tanzania na Uganda zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, usalama, miundombinu na ushirikiano wa kikanda, hali ambayo imechangia maendeleo ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kwa mujibu wa Balozi Shelukindo, vikao vya JPC ni jukwaa muhimu la kujadili na kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili pamoja na kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha nne kilichofanyika mwaka 2022.

Aidha, amewapongeza viongozi wakuu wa nchi hizo, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda, kwa kuendelea kutoa mwelekeo na msukumo katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo.

Katika kikao hicho, wajumbe kutoka pande zote mbili wanatarajiwa kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo masuala ya kisiasa na kidiplomasia, amani na usalama, biashara na viwanda pamoja na kuimarisha uhusiano wa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kikao hicho pia kinatarajiwa kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kikao kilichopita na kubaini fursa mpya za ushirikiano zitakazochangia kukuza uchumi, kuimarisha amani na kudumisha mahusiano ya kirafiki kati ya Tanzania na Uganda.