Breaking News

MCHUNGAJI MWAIFWANI AKEMEA UPOTOSHAJI NA SHINIKIZO KWA TUME YA UCHUNGUZI

Na Mwandishi Wetu - Mchungaji John Mwaifwani wa Kanisa la Pentekoste Boanerge ametoa onyo kali dhidi ya mwenendo unaojitokeza miongoni mwa wanaharakati na watengeneza maudhui mitandaoni, wanaojaribu kushawishi maoni ya umma kuhusu Tume ya Jaji Chande. Amesema hatua hiyo inaweza kuhatarisha uadilifu na uhuru wa mchakato wa uchunguzi unaoendelea.

Akizungumza jijini dar es salaam Mchungaji Mwaifwani alisisitiza kuwa si sahihi kwa makundi au watu binafsi kuanza kutoa hitimisho au kulazimisha mitazamo yao kabla ya tume hiyo kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti rasmi.

Alieleza kuwa kumekuwa na ongezeko la matumizi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara kushinikiza mwelekeo fulani wa majibu kutoka kwa tume hiyo. Kwa mujibu wake, hali hii ni hatari kwa mustakabali wa haki na amani ya taifa.

“Ni muhimu kuitambua tume hii kama chombo huru kilichoundwa kuchunguza kwa kina matukio yaliyojitokeza tarehe 29 Oktoba, wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Inapaswa kuachiwa nafasi ya kufanya kazi yake bila kuingiliwa,” alieleza.

Aidha, mchungaji huyo amewataka wananchi kuwa na subira na kuamini mchakato wa uchunguzi unaoendelea. Alibainisha kuwa haki ya kweli hupatikana pale taasisi husika zinapofanya kazi kwa uhuru, bila shinikizo la nje.

Katika tahadhari yake, alionya dhidi ya kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho au zenye lengo la kupotosha umma, akisema kuwa vitendo hivyo vinaweza kuchochea taharuki na kuathiri mshikamano wa kitaifa.

Akigusia matumizi ya mitandao ya kijamii, Mwaifwani alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa watumiaji wake. Alisema uhuru wa kujieleza haupaswi kutumiwa vibaya kwa kuingilia kazi za vyombo halali vya uchunguzi au kupotosha mjadala wa kitaifa.

“Baadhi ya maudhui yanayosambazwa yana dalili za kupotosha ukweli na yanaweza kuharibu mwelekeo wa mjadala juu ya masuala nyeti ya kitaifa,” alionya.

Akihitimisha kwa kuwataka Watanzania kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kuheshimu sheria na taasisi zilizowekwa. Alisisitiza kuwa kuipa tume nafasi ya kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti rasmi kutachangia kupatikana kwa ukweli, haki na maridhiano ya kitaifa.

"Mustakabali wa taifa unategemea nidhamu ya wananchi katika kuheshimu taratibu na kuacha taasisi huru kufanya kazi zake kwa uadilifu na bila kuingiliwa".