Breaking News

RAIS WA KENYA, MHE. WILLIAM RUTO AHUTUBIA BUNGE LA TANZANIA KWA MARA YA KWANZA: ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. William Ruto, ameandika historia Mei 5, 2026 jijini Dodoma kwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, akisisitiza kuimarishwa kwa umoja, ushirikiano wa kikanda, biashara na maendeleo ya pamoja kati ya nchi za Afrika Mashariki.

Katika hotuba yake iliyopokelewa kwa shangwe na wabunge, Mhe. Rais Ruto alieleza kuwa Kenya na Tanzania zina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akihimiza kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa haya mawili na kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na umaskini ili kujiletea maendeleo endelevu yenye manufaa ya watanzania na wakenya.

“Ushirikiano wetu si chaguo bali ni wajibu wa kihistoria kwa ustawi wa watu wetu. Maadui wa Tanzania sio Wakenya na maadui wa Kenya sio Watanzania, Maadui zetu ni ukosefu wa maendeleo, kazi na umaskini. Hivyo tujitahidi kupambana na maadui hawa ili kujiletea maendeleo na kuongeza ajira kwa vijana”alisema Mhe. Ruto.

Mhe. Rais Ruto alieleza pia kuwa hatua ya pamoja ya kuwekeza katika miradi mikubwa ni muhimu kwa nchi za Afrika Mashariki ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya ukanda na kuongeza kuwa Afrika Mashariki ina rasilimali za kutosha, lakini kinachohitajika ni maamuzi ya pamoja na uwekezaji wa kimkakati ili kuzitumia kikamilifu rasilimali hizo.

Moja ya miradi mikubwa iliyotajwa ni ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kusafisha mafuta katika Mji wa Tanga ambacho kinatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa ukanda mzima, kwani kitahakikisha mafuta ghafi yanachakatwa ndani ya nchi badala ya kusafirishwa nje.

Mhe. Rais Ruto alieleza kuwa uchaguzi wa kuamua kuiunga mkono Tanga unatokana na uwepo wa miundombinu muhimu kama Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambalo litarahisisha usafirishaji na usambazaji wa mafuta.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azan Zungu, alimshukuru Mhe. Rais Ruto kwa hotuba yake ambayo alisema imeakisi dhamira ya kweli ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Kenya.