Breaking News

TANESCO YAENDELEA KUIMARISHA MATUMIZI YA TEHAMA KUBORESHA HUDUMA

Na  Woinde Shizza, Arusha - Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kuonesha dhamira yake ya kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani kwa kuandaa Jukwaa la TEHAMA (ICT Forum 2026) linalofanyika  jijini Arusha, likilenga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mkurugenzi wa ICT wa TANESCO, David Bondo, alisema kongamano hilo limebeba kaulimbiu isemayo “Modern ICT for a Smarter TANESCO”, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo kuhakikisha teknolojia za kisasa zinatumika kuongeza ufanisi wa kazi na kuboresha huduma kwa wateja.

Alisema kupitia jukwaa hilo, wataalamu wa TEHAMA kutoka ndani  ya shirika wanapata nafasi ya kujadili mbinu mbalimbali za kidijitali zinazoweza kusaidia kuboresha utendaji kazi wa TANESCO sambamba na kuimarisha sekta ya nishati nchini.

“Mageuzi ya kidijitali ni sehemu muhimu katika kuhakikisha huduma za TANESCO zinakuwa za haraka, salama na zenye kuaminika zaidi kwa wananchi tunataka kwenda sambamba na kasi ya teknolojia duniani,” alisema Bondo.
.Bondo alisema matumizi ya mifumo ya kisasa ya TEHAMA yameendelea kusaidia shirika hilo kuboresha huduma kwa wateja, kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma pamoja na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi kupitia mifumo ya kidijitali.

Alisema Miongoni mwa mada zinazojadiliwa katika kongamano hilo ni mageuzi ya kidijitali katika sekta ya huduma, usimamizi wa takwimu na ubora wa data, matumizi ya mifumo ya wingu (Cloud Systems) pamoja na uboreshaji wa vituo vya kisasa vya kuhifadhi taarifa.

 Alibainisha  pia wanajadili masuala ya usalama wa mtandao na ulinzi wa miundombinu muhimu, ubunifu wa TEHAMA pamoja na teknolojia mpya zinazoibukia duniani huku wakitathmini namna bora ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya kidijitali.
Naye Mratibu wa Mradi wa Maboresho ya Mifumo ya TEHAMA, Demitruce Dashina, alisema jukwaa hilo ni muhimu katika kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya na kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuimarisha sekta ya nishati kupitia matumizi sahihi ya TEHAMA.

Alisema matumizi ya mifumo ya kisasa yataisaidia TANESCO kuongeza ubora wa huduma, kupunguza changamoto za kiutendaji pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya shirika na wateja

Alibainisha kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaendelea kusaidia kuboresha utendaji kazi ndani ya TANESCO kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa haraka, kuongeza ufanisi wa kazi pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya shirika na wateja.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa watumishi na wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mifumo hiyo ili kuongeza uelewa na matumizi yake kwa ufanisi zaidi.

Jukwaa hilo limewakutanisha wataalamu wa TEHAMA,ambapo wanatarajiwa kujadili kwa kina mchango wa teknolojia katika kuleta maendeleo ya huduma za umeme nchini.