Breaking News

ACT-WAZALENDO YAPOKEA WANACHAMA 128 WA VYUO VIKUU JIJINI DAR

Dar es salaam - Chama cha ACT-Wazalendo kimepokea wanachama wapya 128 kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu mkoani Dar es Salaam, hatua ambayo viongozi wa chama hicho wameitaja kuwa ishara ya kuongezeka kwa imani ya vijana kwa chama hicho na harakati zake za kudai haki, demokrasia na utawala bora nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema chama kimeamua kuwapokea wanachama hao kwa heshima maalum kutokana na nafasi muhimu ambayo wanafunzi wa vyuo vikuu wanayo katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kisiasa nchini.

Alisema tofauti na ilivyo kawaida ambapo wanachama wapya hupokelewa katika matawi yao, safari hii viongozi wa juu wa chama waliamua kuwakaribisha rasmi vijana hao kutokana na umuhimu wa kundi hilo katika mapambano ya maendeleo na demokrasia.

“Heshima hii haijaja kwa bahati mbaya. Chama kinaelewa nafasi nyeti na mchango mkubwa wa wanafunzi wa vyuo vikuu katika mapambano ya ukombozi wa taifa. Hadi sasa wanachama wapya 128 wamejiandikisha kujiunga na chama chetu,” alisema Ado Shaibu.

Alieleza kuwa hatua ya vijana hao kujiunga na ACT-Wazalendo kwa hiari yao wenyewe ni jambo la kipekee na la kutia moyo, kwani mara nyingi vyama hulazimika kufanya kampeni za kuwashawishi wananchi kujiunga.

Katibu Mkuu huyo alitoa wito kwa Ngome ya Vijana ya chama kuhakikisha wanachama hao wanakuwa mabalozi wa kusambaza fikra za mabadiliko katika vyuo vikuu vya Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.

Ado Shaibu pia alisisitiza nafasi ya wanawake katika harakati za ukombozi wa jamii, akieleza kuwa hakuna mapinduzi ya kijamii yanayoweza kufanikiwa bila ushiriki wa wanawake.

“Wanawake wana nafasi ya kipekee katika mapambano ya kijamii. Historia inaonyesha kuwa mafanikio ya harakati nyingi duniani yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na wanawake,” alisema.

Katika hotuba yake, Ado Shaibu alieleza kuwa jukumu kuu la chama cha siasa ni kutetea maslahi ya wananchi na si ya viongozi au wanachama wake pekee. Alisema ACT-Wazalendo itaendelea kusimamia uwajibikaji wa viongozi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupigania demokrasia, haki za binadamu, katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, akisema hayo ni mambo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, alisema ujio wa vijana hao unaonyesha kiu ya kizazi kipya kuona Tanzania yenye haki, usawa, demokrasia na uongozi bora.

Alisema vijana hawa wameamua kujiunga na jukwaa ambalo kwa muda mrefu limekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi na kupaza sauti dhidi ya changamoto zinazowakabili vijana na wanafunzi nchini.

“Maamuzi yenu ya kujiunga na ACT-Wazalendo yanaonyesha dhamira ya kuona Tanzania inayotumia rasilimali zake kwa manufaa ya wananchi wote na si kwa maslahi ya wachache,” alisema Nondo.

Alisisitiza kuwa siasa huathiri maisha ya kila mwananchi na kwamba vijana hawawezi kujitenga na masuala ya kisiasa kwa kuwa maamuzi ya serikali na taasisi mbalimbali huathiri moja kwa moja maisha yao ya kila siku.

Nondo alieleza kuwa Ngome ya Vijana imekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, ikiwemo kuhamasisha ongezeko la bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, kupinga baadhi ya tozo zinazowakabili wanufaika wa mikopo na kushinikiza kuboreshwa kwa ustawi wa vijana nchini.

Pia aliibua suala la wanafunzi 17 wanaokabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka ili kupata mikopo ya elimu ya juu, akitaka serikali kuiondoa kesi hiyo na kutafuta suluhu ya haki kwa wanafunzi hao.

“Tunaiomba serikali kuachana na kesi hiyo na kuangalia kwa kina mazingira yaliyowasukuma wanafunzi hao kufikia hatua hiyo. Vijana wanahitaji kusaidiwa na kusikilizwa,” alisema Nondo.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa kukabidhiwa kadi za uanachama kwa baadhi ya wanachama wapya huku viongozi wa chama wakiahidi kuendelea kushirikiana na vijana katika harakati za kuimarisha demokrasia, haki na maendeleo nchini.