AfDB NA ASSA WASAINI MKATABA WA KUIMARISHA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU AFRIKA
Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Jumuiya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi za Afrika (ASSA) zimesaini mkataba wa ushirikiano utakaowezesha mifuko ya hifadhi ya jamii barani Afrika kushiriki kwa ufanisi katika uwekezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu ya kiuchumi na kijamii.
Lengo la ushirikiano huo ni kuimarisha ukwasi na uhimilivu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, kuboresha huduma na mafao kwa wanachama wake, pamoja na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa bara la Afrika.
Makubaliano hayo yalitiwa saini katika kilele cha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa AfDB uliofanyika Mei 28, 2026, jijini Brazzaville, Congo. Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu wa ASSA, Meshach Bandawe, pamoja na Mkurugenzi wa Sekta ya Fedha wa AfDB, Ahmed Attout, na kushuhudiwa na Rais wa AfDB, Dk. Sidi Ould Tah.
Kupitia ushirikiano huo, pande hizo mbili pia zitashirikiana katika kujenga uwezo wa sekta ya hifadhi ya jamii Afrika, ikiwemo kutoa msaada wa kiufundi ili kuongeza wigo wa watu wanaonufaika na huduma za hifadhi ya jamii.
Aidha, makubaliano hayo yanakusudia kuhamasisha matumizi ya rasilimali na mapato ya ndani ya nchi za Afrika katika uwekezaji wa miradi ya miundombinu yenye tija kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na wanachama wake, huku ikichangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuunda ajira, kupunguza umaskini, kuongeza pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
Licha ya changamoto ya nakisi ya miundombinu, Afrika inaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo usafirishaji kupitia barabara, reli, viwanja vya ndege na bandari, pamoja na sekta za nishati, mawasiliano ya kidijitali, viwanda na kilimo. Uwekezaji huo unalenga kuimarisha muunganiko wa kibiashara wa kikanda kama ilivyoainishwa katika Ajenda ya Kijamii ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2026.
ASSA ilianzishwa nchini Rwanda huku makao yake makuu yakihamishiwa jijini Arusha, Tanzania. Jumuiya hiyo inalenga kuwezesha mifuko ya hifadhi ya jamii Afrika kufanya kazi kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo upanuzi wa wigo wa wanachama, mifumo ya utendaji, sera na miongozo ya hifadhi ya jamii, maboresho ya mafao, uwekezaji na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma.
Hivi karibuni, Kamati ya Utendaji ya Mawaziri wa Sekta za Miundombinu na Nishati ya Umoja wa Afrika (AU) ilipitisha azimio la kuendelea kuiimarisha ASSA ili kuongeza ufanisi wa shughuli zake katika bara la Afrika.





