BUDDHA WAIISIFU TANZANIA KWA KUENDELEA KUDUMISHA AMANI NA UHURU WA KUABUDU
Dar es salaam - Kiongozi Mkuu wa dini ya Buddha nchini, Dkt. Ilukuptiye Pannasekara, ameisifu Tanzania kwa kuendelea kudumisha uhuru wa kuabudu pamoja na ushirikiano mzuri kati ya dini mbalimbali na Serikali.
Dkt. Pannasekara alitoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Kiongozi wa dini ya Buddha duniani, yaliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 106 tangu kuanzishwa kwa Hekalu la kwanza la Buddha nchini, Golden Buddha House, lililopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Amesema waumini wa dini ya Buddha nchini wameendelea kufurahia mazingira ya amani na utulivu kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa dini nyingine na Serikali.
“Mara zote tumekuwa tukipata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na waumini wa dini mbalimbali nchini, jambo linalotufanya tuishi kwa amani, upendo na mshikamano,” amesema Dkt. Pannasekara.
Katika hafla hiyo, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Deus Sangu, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na dini zote bila ubaguzi, kwa lengo la kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Amesisitiza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika kuhamasisha maadili mema, kuimarisha amani na kuchochea maendeleo ya jamii







