SERIKALI KUFANYA TATHMINI YA KILA MWAKA ILI KUKUZA MCHANGO WA SEKTA BINAFSI- DKT. CHAYA
Serikali imepanga kuanzisha utaratibu wa kufanya tathmini ya kila mwaka ili kufuatilia mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa Taifa, hatua inayolenga kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kufikia lengo la uchumi wa dola za Marekani trilioni moja.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, alipokuwa akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 22, 2026.
Dkt. Chaya amseema chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imejipanga kuleta mabadiliko makubwa kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kwa kutumia mbinu mpya za kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema mwaka huu Serikali imeanza kutumia mfumo wa Phase Out Approach (utaratibu wa kukamilisha kwanza miradi iliyoanza kabla ya kuanzisha mingine mipya) ili kuhakikisha miradi iliyopo inakamilika na kuanza kutoa tija kwa wananchi.
“Tumekuja kivingine. Tunataka kuhakikisha miradi ambayo tayari imeanza, iwe ya kilimo, maji au sekta nyingine, inakamilishwa kwanza na kuanza kuleta matokeo kabla ya kuendelea na miradi mingine,” alisema Dkt. Chaya.
Ameeleza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo Serikali inatarajia kupata mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, bajeti za kila mwaka pamoja na mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta mbalimbali.
Aidha, amesema Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji itafanya Mid-Year Review (tathmini ya utekelezaji katikati ya mwaka) ili kupima maendeleo yaliyofikiwa, kubaini mafanikio na changamoto pamoja na kujifunza maeneo yanayohitaji maboresho kuelekea mwaka 2030.
Dkt. Chaya amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia kupunguza baadhi ya tozo na kufanya maboresho mbalimbali ya sera na mifumo ya kiuchumi ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika kuvutia wawekezaji.
Amesema kwa kuwa, Dira ya Taifa 2050 imeeleza wao kuwa asilimia 70 ya uchumi wa Taifa urachangiwa na sekta binafsi, na hivyo Serikali imeamua kuelekeza nguvu kubwa katika sekta za uzalishaji ambazo ndizo zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya wananchi.
“Rais ameshatuagiza sisi na Mawaziri wote kuhakikisha nguvu zetu na akili zetu tunazipeleka katika sekta za uzalishaji kwa sababu huko ndiko tutakakotengeneza ajira nyingi zaidi kwa Watanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Dkt. Chaya, jukumu kubwa la Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kutumia maeneo ambayo bado hayajatumika kikamilifu, ikiwemo mashamba makubwa na viwanda ambavyo havifanyi kazi kwa sasa.
Pia amesema kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Serikali itaendelea kuimarisha huduma za After Care Service (huduma za ufuatiliaji na utatuzi wa changamoto za wawekezaji baada ya kuwekeza) ili kuongeza ufanisi na kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
Dkt. Chaya amebainisha kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na wizara mbalimbali za kisekta itaandaa mwongozo maalum utakaowezesha kufanyika kwa tathmini za kila mwaka za mchango wa sekta binafsi katika uchumi.
Amesema tathmini hizo zitasaidia kubaini maeneo yanayofanya vizuri na yale yenye changamoto ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Tunataka kujua kwa usahihi jinsi sekta binafsi inavyochangia katika uchumi wetu, maeneo gani yanafanya vizuri na yapi yanahitaji kuongezewa nguvu ili yaweze kufanya vizuri zaidi,” alisema Dkt. Chaya.




