SHEIKH JALALA AONYA DHIDI YA KUVURUGA UMOJA WA KITAIFA
Kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini, Sheikh Hemed Jalala, amewahasa Watanzania kuendelea kuuenzi na kuudumisha umoja wa kitaifa, akisisitiza kuwa ni tunu muhimu ambayo taifa halipaswi kuja kuijutia kwa kuipoteza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Sheikh Jalala alisema hakuna changamoto, maneno au tofauti za aina yoyote zinazopaswa kuvuruga umoja na mshikamano ambao Watanzania wameujenga kwa miaka mingi.
Alisema maandiko mbalimbali ya dini, ikiwemo Qurani Tukufu pamoja na vitabu vingine vya dini, yanasisitiza kwa nguvu umuhimu wa umoja, mshikamano na amani katika maisha ya mwanadamu.
"Jambo la kwanza linalosisitizwa katika maandiko ni umoja na mshikamano. Jambo la pili ni kuenzi amani. Hata pale watu wanapodai haki zao au kutafuta wanachostahili, ni muhimu kufanya hivyo kwa njia inayolinda na kudumisha amani ya nchi," alisema.
Sheikh Jalala alieleza kuwa Watanzania wamejaliwa upendo wa kipekee ambao si rahisi kuupata katika mataifa mengi duniani, akibainisha kuwa wananchi wa dini tofauti wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani na mshikamano.
"Ni jambo la kawaida nchini Tanzania kukuta katika mtaa mmoja wanaishi Wakristo, Waislamu na watu wa imani mbalimbali kwa upendo mkubwa. Hata ndani ya familia unaweza kukuta mtu anaitwa Juma Agostino, jambo linaloonesha namna Watanzania walivyojenga mahusiano ya upendo na kuheshimiana," alisema.
Akizungumzia umuhimu wa maadili na tabia njema kwa vijana, Sheikh Jalala alisema hayo ni nguzo muhimu katika kuimarisha maendeleo ya taifa na kudumisha mshikamano wa wananchi.
Alionya kuwa kuvunjika kwa umoja na mshikamano kunaweza kusababisha migawanyiko inayoweza kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.
Aidha, aliwataka Watanzania waepuke juhudi zozote za kugawanywa kwa misingi ya kisiasa, kidini au kikabila, akisema hatua hiyo inaweza kuondoa tunu kubwa ya umoja na mshikamano ambayo taifa limebarikiwa kuwa nayo.
"Nitoe rai kwa Watanzania, hususan vijana, kutambua kuwa amani tuliyonayo ni hazina kubwa. Ushirikiano uliopo kati ya Waislamu na Wakristo nchini ni mfano mzuri unaoonesha kuwa Tanzania haina ubaguzi wa kidini wala ukandamizaji wa aina yoyote," alisema.
Sheikh Jalala alisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani, umoja na mshikamano ni la kila Mtanzania bila kujali dini, kabila au itikadi za kisiasa.




