VIJANA WAHIMIZWA KULINDA AMANI NA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Juma Simba, amewahimiza vijana wa wilaya hiyo kuendelea kulinda amani ya taifa ili kuweka mazingira bora yatakayowezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform), DC Simba alisema amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.
Alieleza kuwa jukwaa hilo limeanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha vijana kutoka makundi mbalimbali ili kujadili masuala yanayowahusu, kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili katika nyanja za kijamii na kiuchumi.
“Vijana wanapaswa kuwa walinzi wa amani na utulivu wa nchi yetu. Tunapokuwa na amani, kila mmoja anapata fursa ya kufanya kazi, kuendesha biashara na kushiriki katika shughuli za maendeleo,” alisema Simba.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Salim Hashim, aliwataka vijana kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zinazotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.
Mbunge huyo alisema ofisi yake imeandaa mpango maalumu wa kuwawezesha vijana kupitia mikopo isiyokuwa na riba ili kuwasaidia kukuza na kuendeleza biashara zao, hatua inayolenga kuongeza ajira na kuinua vipato vya vijana katika jimbo hilo.
Aliwahimiza vijana kuwa wabunifu, wachapakazi na kutumia vyema fursa zilizopo ili kujijengea maisha bora na kuchangia maendeleo ya jamii pamoja na taifa kwa ujumla.
Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushiriki wa vijana katika masuala ya maendeleo, huku ukiwawezesha kupata taarifa, elimu na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana ndani na nje ya wilaya hiyo.




