Breaking News

WANANCHI MBWENI WAPANIA KUISHTAKI SERIKALI

Diwani wa Kata ya Mbweni, Abdul Mgheni, akitoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu malalamiko ya matumizi mabaya ya maeneo ya huduma za jamii na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa. Picha na Moses Mwakibolwa.


Dar es salaam - Maelfu ya wananchi wa Mtaa wa Malindi Estate, Wilaya ya Kinondoni, wameazimia kuiburuza mahakamani Serikali kwa madai ya kugawa maeneo ya umma kwa watu binafsi bila kufuata taratibu za kisheria.

Katika kutekeleza azma hiyo, wananchi hao wameunda kamati ya watu tisa itakayofuatilia na kuchunguza taratibu zinazotumiwa na maofisa ardhi wa Wilaya ya Kinondoni katika ugawaji wa maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma.

Katika mkutano wa wananchi uliofanyika wiki iliyopita, ilielezwa kuwa baadhi ya viwanja vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya shule, soko, kituo cha daladala na taasisi za kifedha vimepimwa kwa lengo la kugawiwa watu binafsi wanaodaiwa kuwa vigogo serikalini.

Wananchi hao walidai kuwa hatua hiyo imefanyika bila kuzingatia umuhimu wa maeneo hayo kwa jamii, huku baadhi yake yakiwa karibu na hospitali na kituo cha polisi.

Diwani wa Kata ya Mbweni, Abdul Mgheni, ambaye alihudhuria mkutano huo, alieleza kusikitishwa na madai ya ukiukwaji wa taratibu hizo na kuahidi kutoa ushirikiano katika kufuatilia suala hilo katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Selina Mkony, alisema ofisi yake haikushirikishwa katika zoezi hilo. Alidai kuwa alipowauliza maofisa ardhi waliokuwa wakiweka alama kwenye maeneo husika, walimweleza kuwa walikuwa wakitekeleza maelekezo kutoka mamlaka za juu.

Naye Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa kufuatilia suala hilo, Wakili Richard Mbaruku, alisema uchunguzi umeanza ili kubaini ukweli wa madai hayo. Aliongeza kuwa endapo Serikali haitatoa majibu ya kuridhisha, wananchi wako tayari kufungua kesi mahakamani.

Hii ni mara ya pili kwa viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kutuhumiwa kuhusika na migogoro ya ardhi katika Mtaa wa Malindi Estate. Awali, kulikuwa na malalamiko kuhusu vigogo kujenga maghorofa kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya makaburi.

Wananchi walitoa wito kwa Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kuingilia kati suala hilo ili kulinda maslahi ya umma.

Juhudi za kumpata Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukurani Kyando, kwa ajili ya kuzungumzia madai hayo hazikufanikiwa, baada ya simu yake kuita bila kupokelewa