Breaking News

WIPO, BRELA NA COSTECH WAZINDUA MRADI WA KUIMALISHA KILIMO NA UFUGAJI KWA TEKNOLOJIA ZA HAKIMILIKI

Dar es salaam - Shirika la Kimataifa la Haki Miliki, World Intellectual Property Organization (WIPO), kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, wamezindua mradi wa miezi 12 unaolenga kutumia teknolojia zilizopo katika kanzidata za kimataifa za hakimiliki kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha sekta za kilimo na ufugaji nchini.

Mradi huo unalenga kutambua, kuchambua na kuhamisha teknolojia ambazo muda wake wa ulinzi wa hakimiliki umeisha kupitia kanzidata za WIPO, ili ziweze kuboreshwa kulingana na mazingira na mahitaji ya Tanzania kwa manufaa ya wakulima, wafugaji na sekta ya viwanda
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Juni 1, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya uchumi, hususan katika sekta za kilimo na ufugaji.

Alisema mradi huo utawezesha wataalamu na wabunifu wa ndani kupata teknolojia sahihi zinazoweza kuboreshwa na kutumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo, uchakataji wa mazao pamoja na maendeleo ya viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo.
“Mradi huu utajikita katika kutafuta teknolojia zinazofaa mazingira ya Tanzania kupitia kanzidata za WIPO. Teknolojia hizo zitafanyiwa maboresho kulingana na mahitaji ya ndani na kutumika kuandaa mifano ya mashine na vifaa vitakavyosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa za kilimo,” alisema Dkt. Nungu.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza utegemezi wa teknolojia ghali kutoka nje ya nchi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mchango wa ubunifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Loy Mhando, alisema mradi huo utasaidia kutumia taarifa zilizopo katika kanzidata za kimataifa za hakimiliki kutafuta teknolojia zinazoweza kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji.

Alieleza kuwa maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na teknolojia za uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo, hatua ambayo itasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kuboresha uzalishaji katika sekta ya mifugo nchini.