DKT. KITABUPAZI ATOA DARASA LA HOMA YA INI, AHIMIZA UPIMAJI WA MAPEMA
Dar es Salaam - Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima homa ya ini mapema ili kubaini maambukizi na kupata matibabu kwa wakati, hatua itakayosaidia kupunguza madhara makubwa ikiwemo ugonjwa wa ini kusinyaa na saratani ya ini.
Wito huo umetolewa na Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini na Mkuu wa Kitengo hicho katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Aswile Kitabupazi, wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika sambamba na kambi ya upimaji na utoaji chanjo katika maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani.
Dk. Kitabupazi alisema maadhimisho hayo hufanyika Julai 28 ya kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa wa homa ya ini, njia za maambukizi, kinga na matibabu.
Alisema siku hiyo ilianzishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa heshima ya mwanasayansi Baruch Samuel Blumberg, aliyegundua virusi vya homa ya ini aina ya B mwaka 1967 na baadaye kutunukiwa Tuzo ya Nobel mwaka 1976 kutokana na mchango wake katika sayansi ya tiba.
"WHO ilitenga siku hii ili kuhamasisha jamii duniani kutambua umuhimu wa kupima, kujikinga na kutibiwa mapema dhidi ya homa ya ini," alisema.
Alifafanua kuwa homa ya ini aina ya B husababishwa na virusi vinavyoshambulia ini na huambukizwa kupitia njia kuu nne ambazo ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au kunyonyesha, kujamiiana bila kinga, kuongezewa damu isiyo salama pamoja na matumizi ya vifaa vyenye ncha kali vilivyochafuliwa na damu yenye maambukizi.
Kwa mujibu wa Dk. Kitabupazi, tafiti zinaonyesha kuwa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ndiyo chanzo kikubwa zaidi cha kuenea kwa virusi vya homa ya ini aina ya B.
"Mama mwenye virusi anaweza kumwambukiza mtoto akiwa tumboni, wakati wa kujifungua au baada ya kuzaliwa. Hii ndiyo njia kubwa zaidi ya maambukizi na ndiyo sababu tunasisitiza wajawazito kupimwa mapema," alisema.
Alisema watu wazima wanaopata maambukizi kupitia kujamiiana mara nyingi huwa na uwezo wa kuondoa virusi hivyo wenyewe kutokana na kinga ya mwili, ambapo zaidi ya asilimia 80 hupona ndani ya kipindi cha miezi sita.
Hata hivyo, alieleza kuwa baadhi ya wagonjwa hushindwa kuondoa virusi hivyo na huingia katika hatua ya maambukizi sugu (Chronic Hepatitis B), hali inayoongeza hatari ya kupata uharibifu wa ini na saratani.
Dk. Kitabupazi alisema ugonjwa huo huendelea kwa hatua mbalimbali kuanzia ini kuwa gumu (fibrosis), kusinyaa (cirrhosis) na baadaye kupata saratani ya ini endapo mgonjwa hatapata matibabu na ufuatiliaji wa karibu.
Alisema dalili za awali za homa ya ini mara nyingi hufanana na mafua ya kawaida, ikiwemo homa ndogo, maumivu ya viungo, uchovu na kukosa nguvu, hali inayowafanya watu wengi kutotambua kuwa wameambukizwa.
"Dalili hizi huwafanya wengi kudhani wana malaria au mafua ya kawaida, hivyo hupuuza kupima afya zao. Wengine hufika hospitalini ugonjwa ukiwa umefikia hatua za mwisho," alisema.
Aliongeza kuwa ugonjwa unapokuwa umeendelea, mgonjwa anaweza kupata macho ya njano, tumbo kujaa maji, kupungua uzito, kudhoofika kwa misuli na kushindwa kufanya kazi za kawaida kutokana na ini kushindwa kutekeleza majukumu yake.
Kuhusu matibabu, Dk. Kitabupazi alisema wagonjwa wenye maambukizi ya muda mfupi (Acute Hepatitis B) hufuatiliwa kwa miezi sita kwa kuwa wengi hupona bila kutumia dawa.
Alisema wagonjwa wenye maambukizi sugu hupimwa kwa kutumia vipimo mbalimbali ikiwemo Ultrasound, CT Scan, APRI Score na vipimo vya utendaji wa ini ili kubaini kama wanahitaji kuanza dawa.
"Endapo ini limeanza kusinyaa au vipimo vinaonyesha uharibifu mkubwa, mgonjwa anaweza kuhitajika kutumia dawa kwa muda mrefu au maisha yote," alisema.
Aidha, alisema wanawake wajawazito wanaobainika kuwa na virusi vya homa ya ini hupewa dawa ili kupunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto.
Alifafanua kuwa mtoto anayezaliwa na mama mwenye maambukizi anatakiwa kupewa kinga maalumu (Immunoglobulin) ndani ya saa 72 baada ya kuzaliwa pamoja na chanjo zote za kawaida zinazolinda dhidi ya homa ya ini.
Kwa mujibu wake, watoto wanaopata chanjo utotoni hulindwa kwa muda mrefu, lakini wanashauriwa kupima kiwango cha kinga wanapokuwa watu wazima ili kubaini kama wanahitaji dozi ya nyongeza (Booster Dose).
Akizungumzia imani potofu zilizopo katika jamii, Dk. Kitabupazi alisema homa ya ini haiambukizwi kwa kushikana mikono, kugusana, kula pamoja, jasho wala mate.
"Jamii inapaswa kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya homa ya ini kwa sababu njia hizo si chanzo cha maambukizi," alisema.
Alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Vunja", inayolenga kuondoa vikwazo vinavyowazuia wananchi kupata huduma za upimaji, kinga na matibabu pamoja na kupambana na taarifa potofu kuhusu ugonjwa huo.
Akitoa takwimu za ugonjwa huo, Dk. Kitabupazi alisema zaidi ya watu milioni 500 duniani wanaishi na virusi vya homa ya ini, huku takribani watu milioni 1.3 wakifariki kila mwaka kutokana na madhara ya ugonjwa huo.
Alisema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa sasa inahudumia takribani wagonjwa 5,000 katika kliniki ya homa ya ini, huku zaidi ya wagonjwa 100 wakihudhuria huduma hizo kwa kila kliniki na wagonjwa wawili hadi watatu wakilazwa kila siku kutokana na matatizo ya ini.
"Changamoto kubwa tuliyonayo ni wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa wamechelewa. Hali hiyo hupunguza nafasi ya matibabu kufanikiwa na kuongeza hatari ya kupata saratani ya ini," alisema.
Aliwataka wananchi wanaogundulika kuwa na maambukizi ya homa ya ini kubadili mtindo wa maisha kwa kuacha matumizi ya pombe, kudhibiti uzito, kula lishe bora na kuhudhuria kliniki kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara.
Akihitimisha, Dk. Kitabupazi aliwahimiza Watanzania kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara badala ya kusubiri dalili kujitokeza, akisema hatua hiyo ndiyo njia bora ya kujikinga dhidi ya madhara makubwa ya homa ya ini.
"Afya ni mtaji wa maisha. Kupima mapema kunatoa nafasi kubwa ya kuzuia ugonjwa usifikie hatua hatarishi na kuokoa maisha ya wengi," alisema.




