NONDO: KAULI YA NCHIMBI KUHUSU KATIBA MPYA YAZUA MASWALI YA DHAMIRA YA SERIKALI
Dar es Salaam. Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo imesema kauli ya Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kuhusu mchakato wa Katiba Mpya imeibua maswali kuhusu dhamira ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kutekeleza ahadi ya kuhuisha mchakato huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ya ACT Wazalendo, Abdul Omary Nondo, alisema kauli ya Makamu wa Rais iliyotolewa Julai 24, 2026, kwamba Serikali, Rais Samia Suluhu Hassan na CCM wanataka Katiba Mpya, huku akiwataka wananchi "kupambana" ili kuipata, inaonekana kuwa na mkanganyiko wa kimantiki.
Nondo alisema ikiwa Serikali na CCM kwa pamoja wanaunga mkono upatikanaji wa Katiba Mpya, bado kunabaki swali la nani anayepaswa kushinikizwa au kupingwa ili mchakato huo uanze.
Alisema Makamu wa Rais hawezi kutenganishwa na Serikali wala CCM kwa kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ndiye msaidizi mkuu wa Rais, hivyo kauli yake inapaswa kutafsiriwa kama msimamo wa Serikali.
Kwa mujibu wa Nondo, CCM ilinadi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuwa ingeanzisha mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani. Hata hivyo, alisema kauli ya sasa ya kuwataka wananchi wapambane ili kuipata imezua maswali kuhusu utekelezaji wa ahadi hiyo.
Aidha, alisema hadi sasa hakuna ratiba ya wazi wala bajeti iliyotengwa mahsusi kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya, jambo ambalo, kwa mtazamo wa ACT Wazalendo, linaashiria ukosefu wa dhamira ya dhati.
Nondo alikumbusha kuwa mapendekezo ya kutaka Katiba Mpya yamewahi kutolewa na tume mbalimbali tangu mwaka 1991, zikiwemo Tume ya Jaji Francis Nyalali, Tume ya Jaji Robert Kisanga, Kamati ya Jaji Mark Bomani, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, Kikosi Kazi cha Profesa Rwekaza Mukandala, pamoja na Tume zilizoongozwa na Jaji Othman Chande.
Alisema historia inaonyesha kuwa suala la Katiba Mpya limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu bila kufikia utekelezaji unaotarajiwa.
Pia, aliwataka vijana, vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wananchi kuendelea kushinikiza kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa njia za amani na kwa umoja.




