SANGU: VIONGOZI WASHIRIKIANE BILA KUJALI VYAMA VYAO
Mbunge wa Jimbo la Kwela na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lwanji Tarafa ya Kipeta Sumbawanga ambapo amewasihi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ephraim Konta.
Mbunge wa Kwela na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Nankanga wilaya ya Sumbawanga leo ambapo amewasihi viongozi wa vijiji kushirikiana kwa Diwani wao bila kujali tofauti za kisiasa ili kuchochea maendeleo Picha zote na OWM- KAM
Na OWM (KAM), Sumbawanga - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amewataka viongozi wa vijiji na kata kufanya kazi kwa ushirikiano bila kuzingatia tofauti za vyama vya siasa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.
Akizungumza na wnanchi wa Kijiji cha Nankanga, Tarafa ya Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga leo (21 Julai 2026), Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela, alisema viongozi wanapaswa kuiga mfano wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameunda Serikali inayoshirikisha viongozi kutoka vyama tofauti vya siasa.
Kauli hiyo imekuja baada ya kupokea taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa vijiji katika Kata ya Nankanga hawatoi ushirikiano kwa Diwani wa kata hiyo, Emanuel Saasita Kishangu wa Chama cha NCCR-Mageuzi hali inayodaiwa kuchelewesha upatikanaji wa eneo la kujenga kituo cha afya.
Sangu alisema tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa kikwazo katika kutatua changamoto za wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo yanahitaji mshikamano na ushirikiano wa viongozi wote bila kujali itikadi zao.
Alieleza kuwa hata katika Wizara anayoiongoza, viongozi wenye itikadi tofauti wanafanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuwatumikia Watanzania, akitolea mfano ushirikiano uliopo kati yake na Naibu Waziri, Dkt. Eveline Munisi.
“Mimi ni Waziri ninayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano. Tunafanya kazi kwa pamoja bila kuangalia tofauti za kisiasa kwa sababu lengo letu ni kulitumikia taifa na kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Aidha, alisema wizara yake ina jukumu la kuratibu mahusiano kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo vyama vya siasa na kwamba hivi karibuni alifanya kikao kazi na viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na maridhiano nchini.
Awali, Diwani wa Kata ya Nankanga Emanuel Saasita Kishangu alieleza changamoto zinazoikabili kata hiyo zikiwemo upungufu wa madawati, uchakavu wa miundombinu ya shule za msingi na ukosefu wa kituo cha afya.
Baada ya kusikiliza kero hizo, Sangu alikabidhi madawati 20 yenye thamani ya shilingi milioni mbili kwa Shule ya Msingi Nankanga pamoja na mifuko 100 ya saruji na mabati kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Shule Shikizi ya Nankanga C.
Mbunge huyo pia aliahidi kutoa kitanda cha kujifungulia, godoro na shuka sita kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi hatua inayolenga kuboresha huduma kwa akina mama katika eneo hilo.
Akizungumza na wananchi pamoja na walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nankanga, Sangu aliwataka kuyatunza madawati hayo akisema ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta rasilimali za kumaliza tatizo la wanafunzi kukaa chini, ambapo kwa sasa wanafunzi 242 kati ya 1,546 bado hawana madawati ya kutosha.
Ziara ya Sangu katika Jimbo la Kwela inalenga kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa muhula wa pili kuwa Mbunge na pia kuwapongeza kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.





