UREJESHAJI BORA MKOPO WAWAINUA WALEMAVU KUPATA MKOPO WA MILIONI 75
Na Mwandishi Wetu - Mwenyekiti wa kikundi cha Disabled Group cha Magomeni Mapipa, Mtaa wa Idrisa, Ahmad Issa Kiduka, amesema mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu imewawezesha kujikwamua kiuchumi na kupanua shughuli zao za uzalishaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Uthubutu kwa wanufaika wa mikopo hiyo, Kiduka alisema kikundi chao chenye wanachama watano kilipata mkopo wa Sh milioni 20 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni mwaka 2021, ambao waliutumia kununua bajaji mbili.
Alisema mafanikio yao yalitokana na usimamizi mzuri wa fedha, uwajibikaji na kuzingatia katiba ya kikundi, jambo lililowawezesha kurejesha mkopo wote kwa wakati bila migogoro.
"Baada ya kurejesha mkopo wetu vizuri, tulipata fursa ya kuomba mkopo mwingine wa Sh milioni 75. Kwa sasa kila mwanachama ana bajaji yake na tunaendelea kufanya kazi kwa mafanikio," alisema.
Kiduka alisema kikundi kilikuwa kinakusanya mapato kwa utaratibu, kuyaweka benki na kufanya marejesho kwa wakati, huku pia kikitenga fedha za matengenezo ya bajaji na matumizi ya wanachama.
Alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha makundi maalumu kupitia mikopo hiyo, akisema imeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu wenye ulemavu.
Aidha, aliwataka wanufaika wengine wa mikopo ya halmashauri kuhakikisha wanarejesha fedha kwa wakati ili kutoa nafasi kwa makundi mengine kunufaika na mpango huo.
"Fedha hizi ni za Serikali. Tuzitumie kwa malengo yaliyokusudiwa na tuzirejeshe kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya kuinuka kiuchumi," alisema.




