WAANDISHI WA HABARI WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA NSSF HIFADHI SCHEME
Dar es Salaam – Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewataka waandishi wa habari nchini kujiunga na Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Hiari (NSSF Hiyari Scheme) ili kujenga usalama wa maisha yao baada ya kustaafu na kujikinga dhidi ya changamoto za kiuchumi na kiafya.
Wito huo ulitolewa na Mweka Hazina wa shirikisho la Vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA), James Kalanje, aliyemwakilisha Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, wakati wa ufunguzi wa semina maalum ya kuhamasisha wafanyakazi wa sekta ya habari kujiunga na NSSF Hiyari Scheme, iliyoandaliwa na NSSF kwa wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) jijini Dar es Salaam.
Kalanje alisema sekta ya habari ni nguzo muhimu ya demokrasia, uwazi na maendeleo ya taifa, lakini waandishi wengi, hasa wa sekta binafsi na wanaojitegemea, bado hawapo kwenye mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii jambo linalowaweka katika hatari wanapokumbwa na uzee, maradhi au kushindwa kufanya kazi.
Alisema takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawajajiunga na mifuko rasmi ya hifadhi ya jamii, hali inayowalazimu baadhi yao kutegemea msaada kutoka kwa ndugu na marafiki wanapopata matatizo.
Kalanje alisema NSSF Hiyari Scheme ni fursa muhimu kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na watu waliojiajiri kuweka akiba kulingana na uwezo wao, hatua inayowasaidia kujenga kipato cha uzeeni huku wakipata kinga dhidi ya changamoto mbalimbali za maisha.
Alibainisha kuwa pamoja na akiba ya uzeeni, mpango huo pia unampa mwanachama fursa ya kupata bima ya afya, hivyo kumwezesha kunufaika na huduma za matibabu wakati wa uanachama wake.
Aliwataka wanachama wa JOWUTA kutumia taaluma yao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, huku akisisitiza kuwa wanapaswa kwanza kuwa mfano kwa kujiandikisha wenyewe katika mpango huo.
Aidha, aliwataka waajiri wa vyombo vya habari kuweka mazingira yatakayowahamasisha wafanyakazi wao kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii, akieleza kuwa wafanyakazi wenye uhakika wa maisha ya baadaye huzalisha zaidi na kufanya kazi kwa uaminifu.
Kwa upande wa NSSF, Kalanje aliipongeza kwa kuendelea kutoa elimu kwa wanahabari, lakini akaitaka kuongeza wigo wa kampeni hiyo ili kuwafikia waandishi wa habari na makundi mengine ya sekta isiyo rasmi katika mikoa yote nchini.
Alisema hatua ya kuanza kutoa elimu kwa wanahabari wa Dar es Salaam na Pwani inapaswa kuendelezwa katika maeneo mengine ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na mfumo wa hifadhi ya jamii wa hiari.
Akihitimisha hotuba yake, Kalanje aliwahimiza waandishi wa habari kutochelewa kujiwekea msingi wa maisha yao ya baadaye kwa kujiunga na NSSF Hiyari Scheme, akisisitiza kuwa kuanza kuweka akiba mapema ni njia bora ya kujenga maisha yenye amani, heshima na uhakika baada ya kustaafu.











