CHALAMILA: DAR ES SALAAM YAANZA OPERESHENI KUPUNGUZA FOLENI, MAFURIKO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam - MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu katika mkoa huo, ikiwemo ujenzi wa madaraja na barabara, huku akitangaza hatua mbalimbali za kukabiliana na foleni, mafuriko, ujenzi holela na matumizi yasiyo sahihi ya maeneo ya jiji.
Chalamila amesema Sh27 bilioni zimetolewa kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Jangwani.
Amesema pia Sh17 bilioni pamoja na Sh11 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mengine, akieleza kuwa miradi hiyo inalenga kupunguza tatizo la mafuriko ambalo limekuwa likiathiri wananchi kwa muda mrefu.
“Uongozi lazima ulenge watu na si sifa za muda mfupi. Tunapaswa kuelekeza nguvu kwenye vitu vinavyoishi, vinavyodumu na vinavyogusa Watanzania bila kujali itikadi zao,” amesema Chalamila.»
Amesema Serikali inaendelea na ujenzi na upanuzi wa barabara mbalimbali katika jiji hilo, akieleza kuwa baadhi ya barabara zimechimbuliwa kwa wakati mmoja kutokana na kasi ya utekelezaji wa miradi.
MALORI KUONDOSHWA BARABARANI
Chalamila ametangaza operesheni maalum dhidi ya malori yanayopaki kiholela katika maeneo ya barabara za Dar es Salaam, akisema tabia hiyo ni miongoni mwa sababu zinazochangia foleni katika jiji hilo.
Amesema kuanzia Agosti 17, 2026, hatua zitachukuliwa dhidi ya malori yatakayobainika kupaki katika maeneo yasiyoruhusiwa, yakiwemo maeneo ya barabara kuu.
Amesema malori hayo yataondolewa na kupelekwa katika maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya maegesho.
Kwa mujibu wa Chalamila, Serikali pia inaendelea na majadiliano na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhusu uwezekano wa kuruhusu malori kuingia katikati ya jiji nyakati za usiku pekee, ili kupunguza msongamano wakati wa mchana.
MABASI YA MIKOANI KUONDOKA KATIKATI YA JIJI
Chalamila amesema mabasi ya masafa marefu yanayofanya shughuli za kupakia na kushusha abiria katika maeneo yasiyoruhusiwa katikati ya jiji nayo yataondolewa.
Amesema hadi Agosti 17, 2026, kampuni ambazo hazina vibali vya kuendesha vituo vya mabasi katikati ya jiji zinapaswa kuondoa mabasi yao na kutumia vituo vilivyotengwa.
Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza foleni na kutoa fursa kwa usafiri wa ndani, ikiwemo daladala, bajaji na bodaboda, kuendelea kuhudumia abiria wanaoshuka katika vituo vikuu.
Chalamila amesema Kituo cha Mabasi cha Magufuli kimejengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh5 bilioni na kina uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya mabasi.
Amesema Serikali pia inaangalia uwezekano wa kujenga vituo vingine katika maeneo mbalimbali, ikiwemo upande wa Temeke, ili kupunguza mzigo wa usafiri katika kituo kimoja.
ONYO KWA WAMILIKI WA SILAHA
Katika hatua nyingine, Chalamila ametoa muda hadi Agosti 30, 2026 kwa wamiliki wa silaha halali ambao hawajakamilisha malipo na vibali vinavyotakiwa kisheria kufika katika mamlaka husika na kurekebisha hali hiyo.
Amesema familia za watu waliofariki wakiwa na silaha zinapaswa kuziwasilisha katika kituo cha polisi kilicho karibu ili kupata maelekezo ya namna ya kuzihifadhi wakati taratibu za kisheria na mirathi zikiendelea.
Aidha, amewataka watu wenye silaha zilizopotea au ambazo zimeingia mikononi mwao bila kufuata utaratibu wa kisheria kuzifikisha katika mamlaka husika badala ya kuzificha.
Amesema hatua hizo zinafanyika sambamba na juhudi za kuimarisha usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam.
UJENZI HOLELA WAPEWA ONYO
Chalamila pia amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya ujenzi unaofanyika bila vibali au unaokiuka masharti ya vibali vilivyotolewa.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kisingizio cha maandalizi ya mashindano ya AFCON kujenga kwa haraka bila kuzingatia viwango na taratibu za ujenzi.
Ametoa mfano wa jengo lililoporomoka Kariakoo na kusababisha vifo, akisisitiza kuwa kasi ya ujenzi haiwezi kuwa sababu ya kupuuza usalama.
Amesema timu maalum ya wataalamu kutoka taasisi mbalimbali itahusika katika ukaguzi wa majengo marefu, ikiwemo kubaini kama majengo hayo yamejengwa kwa kuzingatia vibali, idadi ya ghorofa zilizoidhinishwa na viwango vya ujenzi.
Timu hiyo, amesema, itahusisha wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ardhi, Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Wahandisi pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na usimamizi wa ujenzi.
WAGENI WATAKAOFANYA UCHUUZI KUKUMBUSHWA TARATIBU
Chalamila amesema Serikali pia itaanzisha operesheni dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni wanaofanya shughuli za uchuuzi kinyume na masharti ya uwekezaji nchini.
Amesema baadhi ya wageni wamekuwa wakijihusisha na biashara ndogo ndogo ambazo, kwa mujibu wa taratibu za uwekezaji, zinapaswa kuwa fursa kwa Watanzania.
Ametaja biashara kama uuzaji wa nguo, viatu, miwani na bidhaa nyingine kuwa miongoni mwa shughuli ambazo baadhi ya wageni wamekuwa wakifanya kinyume na taratibu.
Amesema kuanzia Agosti 17, 2026, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam itaanza operesheni ya kuhakikisha wafanyabiashara wa kigeni wanafuata masharti ya vibali vyao na kubaki katika shughuli zilizoruhusiwa kisheria.
Kwa wale watakaobainika kukiuka sheria, amesema hatua zitachukuliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Chalamila amesema lengo la hatua hizo si kuzuia uwekezaji wa wageni, bali kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa kufuata sheria na kwamba fursa za biashara ndogo ndogo zinaendelea kuwawezesha Watanzania.
Amesema Serikali inaendelea kushirikisha wataalamu katika kupanga upya jiji la Dar es Salaam ili kukabiliana na changamoto za miundombinu, mazingira, ujenzi holela, usalama na matumizi yasiyo sahihi ya maeneo ya umma




