Breaking News

DMI YATANGAZA FURSA ZA MAFUNZO YA BAHARI KATIKA MAONESHO YA NANENANE

DODOMA: Taasisi ya Bahari Dar es Salaam (DMI) imewahamasisha wananchi, wanafunzi na wadau wa sekta ya uchukuzi wa majini kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Nanenane kupata elimu kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza wataalamu katika sekta ya bahari nchini.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkufunzi Msaidizi wa DMI, Bi. Jacqueline Lema, alisema taasisi hiyo inatoa mafunzo katika ngazi mbalimbali ikiwemo Cheti cha Awali (Basic Technician Certificate), Stashahada, Shahada na Shahada ya Umahiri.

Alisema mbali na programu hizo za muda mrefu, DMI pia hutoa kozi za muda mfupi pamoja na mafunzo ya kitaaluma kwa mabaharia kupitia vyeti vya STCW (Standards of Training, Certification and Watchkeeping).
Bi. Lema aliwataka wananchi, wanafunzi na wadau wa sekta ya uchukuzi wa majini kutembelea banda la DMI katika maonesho hayo ili kupata maelezo kuhusu kozi zinazotolewa, sifa za kujiunga na fursa mbalimbali zinazopatikana chuoni hapo.

Alisisitiza kuwa DMI inaendelea kujikita katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi na umahiri wa kukidhi mahitaji ya sekta ya uchukuzi wa majini nchini na kimataifa.