Breaking News

OLE NGURUMWA: AWATAKA VIJANA KUSIMAMIA MCHAKATO WA KATIBA MPYA

Dar es Salaam - Mkurugenzi wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa, amewataka vijana nchini kuungana na kusimamia kwa nguvu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, akisisitiza kuwa wao ndio kundi kubwa litakaloathirika na manufaa ya Katiba hiyo kwa miaka ijayo.

Akizungumza leo, Agosti 12, 2026, katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Ngome ya Vijana Taifa ya Chama cha ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam, Ngurumwa amesema vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kudai Katiba Mpya bila kujali tofauti za vyama, itikadi au maeneo wanayotoka.

Amesema mchakato huo haupaswi kuanza upya kutoka sifuri, bali Serikali na wadau wanapaswa kutumia nyaraka zilizopo, hususan Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba pamoja na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba, ili kukamilisha mchakato huo.

“Vijana ndio msingi wa upatikanaji wa Katiba Mpya katika taifa letu. Mchakato wetu wa Katiba Mpya haupaswi kuachwa wala kubaki nyuma,” amesema Ngurumwa.

Kwa mujibu wa Ngurumwa, kuanzisha mchakato mpya kabisa kunaweza kuongeza muda wa upatikanaji wa Katiba Mpya, hivyo amewataka vijana kuhakikisha asilimia iliyobaki ya mchakato huo inakamilishwa kwa kutumia msingi uliokwishawekwa.

Amesema vijana wanapaswa kutumia nafasi zao katika makundi na mikusanyiko mbalimbali kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa Katiba Mpya, akisisitiza kuwa suala hilo linawahusu kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwa wao ndio watakaobeba mustakabali wa taifa kwa miongo ijayo.

Ngurumwa pia amewataka Watanzania wanaounga mkono Katiba Mpya kuungana bila kujali vyama vyao vya siasa, itikadi au kanda wanazotoka, ili kujenga nguvu ya pamoja ya kushinikiza kukamilishwa kwa mchakato huo.

“Unganeni kwa pamoja, tengenezeni taratibu za kuwa pamoja wale wote mnaotaka Katiba Mpya,” amesema.

Aidha, amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea haki za binadamu, akisisitiza umuhimu wa vijana kuteteana na kutokubali mtu yeyote kuonewa.

Katika hatua nyingine, Ngurumwa amempongeza kijana Luqman Nondo kwa kusimamia anachoamini na kuwataka vijana wengine kujenga ujasiri wa kusimamia misingi wanayoamini kwa maslahi ya taifa.

Akinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ngurumwa amewataka vijana kuwa jasiri, kujiamini na kupinga mifumo kandamizi, ukandamizaji na ufisadi katika jamii.

Amesema vijana wana nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko nchini na kwamba hatua wanazochukua sasa zinaweza kuwa na athari kubwa katika mustakabali wa Tanzania.