TASAC YAFAFANUA UMUHIMU WA BANDARI KAVU DAR ES SALAAM
DAR ES SALAAM — Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Usimamizi wa Usafiri wa Majini (TASAC), Mohammed Salum, amesema Bandari Kavu (ICD) ni muhimu katika kuimarisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuzuia msongamano wa mizigo, kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa shehena za makontena.
Salum amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum wa kutoa elimu kuhusu sekta ya usafiri wa majini, akieleza kuwa ukuaji wa shehena za makontena umefanya bandari kavu kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa usafirishaji wa mizigo nchini.
Amesema Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa inahudumia zaidi ya makontena 4,000 kwa siku, huku mwezi Julai pekee ikihudumia makontena 137,000.
Kwa mujibu wa Salum, mwaka 2020 bandari hiyo ilihudumia makontena 740,000, lakini mwaka 2025 idadi hiyo iliongezeka hadi makontena 1,245,000, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Amesema ongezeko hilo limetokana kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2021, pamoja na kuingia kwa wawekezaji wapya katika uendeshaji wa bandari.
Salum ameeleza kuwa historia ya ICD inatokana na changamoto ya msongamano wa mizigo iliyojitokeza baada ya ongezeko kubwa la shehena za makontena.
Amesema kabla ya mwaka 2000, shughuli za utunzaji, ukaguzi na uondoshaji wa makontena zilifanyika ndani ya eneo la Bandari ya Dar es Salaam, wakati huo ikiwa ikihudumia takribani makontena 110,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, baada ya kuingia kwa mwekezaji binafsi wa kwanza, TICTS, na kuboreshwa kwa ufanisi wa huduma, idadi ya makontena iliongezeka hadi takribani 340,000 kwa mwaka 2007/2008.
Ongezeko hilo lilisababisha msongamano mkubwa wa mizigo uliosababisha shughuli za bandari kusimama mwishoni mwa mwaka 2007.
Salum amesema hali hiyo ilisababisha Serikali, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wadau wengine, kufanya tathmini na kuamua kuanzisha na kutumia bandari kavu nje ya eneo la bandari ili kupunguza msongamano.
Amesema hatua hiyo ililenga kuifanya Bandari ya Dar es Salaam ijikite zaidi katika jukumu lake la msingi la kushusha na kupakia mizigo kutoka na kwenda kwenye meli, huku shughuli nyingine zikifanyika katika maeneo ya ICD.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza kati ya Desemba na Machi, Salum amesema baadhi ya bandari kavu zilijaa zaidi ya uwezo wake, hali iliyofikia zaidi ya asilimia 150 na kusababisha changamoto katika mtiririko wa mizigo na usafirishaji jijini.
Amesema kutokana na hali hiyo, TASAC kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), iliruhusu kuanzishwa kwa bandari kavu mpya na kubwa zenye eneo la kuanzia mita za mraba 40,000, sawa na takribani ekari 10, ikiwemo Salsala ya Mbagala, Heco ya Kigamboni na KICD.
Hata hivyo, amesema TASAC imechukua hatua za kudhibiti changamoto zinazohusishwa na ongezeko la ICD, ikiwemo kusitisha utoaji wa leseni mpya za bandari kavu mwezi Juni mwaka huu.
Amesema pia TASAC iliitisha kikao cha pamoja na halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam ili kuratibu mipango miji na kubaini maeneo yanayofaa kwa shughuli za bandari kavu.
Kwa sasa, amesema tathmini ya miundombinu inaendelea wakati huu wa msimu wa biashara wenye shehena ndogo, kwa lengo la kujiandaa na ongezeko la mizigo linalotarajiwa kuanza mwezi Oktoba.
Akizungumzia wito wa baadhi ya wadau wa kufungwa kwa ICD au mizigo yote kusafirishwa kwa reli na kupelekwa Kwala, Salum amesema uwezo wa reli na miundombinu iliyopo bado hautoshelezi kubeba shehena yote inayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa ina uwezo wa kuhifadhi takribani makontena 27,000 kwa wakati mmoja, kiasi kinacholingana na siku sita hadi saba za kazi.
Amesema bila kuwa na maeneo ya ziada ya kuhifadhi mizigo nje ya bandari, eneo la bandari linaweza kujaa ndani ya siku chache na kusababisha shughuli za upakuaji na upakiaji wa meli kusimama.
Aidha, amesema reli ya MGR na SGR bado zinaendelea kuboreshwa na kwa sasa hazina uwezo wa kubeba shehena yote ya zaidi ya makontena 4,000 yanayoingia bandarini kwa siku.
Kwa mfano, amesema treni moja ya MGR hubeba takribani makontena 27 kwa safari, hivyo usafirishaji wa mizigo kwa reli pekee hauwezi kukidhi mahitaji yote yaliyopo kwa sasa.
Salum pia amesisitiza umuhimu wa usafiri wa malori katika mfumo wa usafirishaji wa mizigo, akisema malori yanawezesha huduma ya usafirishaji wa mizigo kutoka mlango mmoja hadi mwingine (door-to-door).
Amesema matumizi ya malori ni sehemu ya kawaida ya mifumo ya usafirishaji katika bandari kubwa duniani na kwamba changamoto si kuondoa kabisa usafiri wa malori, bali ni kuhakikisha unaratibiwa kwa ufanisi ili kupunguza kero kwa wananchi na watumiaji wengine wa barabara.
Amewataka waandishi wa habari kuwa mabalozi wa kutoa elimu sahihi kwa umma kuhusu umuhimu wa ICD, akisisitiza kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha uchumi wa Tanzania na nchi jirani zinazotegemea huduma za usafirishaji kupitia bandari hiyo.




