Breaking News

AUMS YAONGEZA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA UCHIMBAJI WA MADINI

Kampuni ya Africa underground mining service (AUMS), inayoshirikiana na kampuni ya Kitanzania, imesema inaendelea kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji wa madini kwa kutumia teknolojia ya uchimbaji chini ya ardhi.

Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita, mwakilishi wa AUMS, Abraham mwakimali amesema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwamo kudhamini Geita Gold FC.

Amesema kampuni hiyo pia imeendelea kutekeleza sera ya local content kwa kutoa ajira kwa Watanzania na kutumia kampuni za ndani katika manunuzi, ambapo asilimia 98 ya manunuzi yake hufanyika ndani ya Tanzania.

Kwa mujibu wa mwakimali, AUMS pia imefungua kituo cha mafunzo Geita kwa kushirikiana na VETA Mwanza, kinacholenga kuwapatia vijana wa Kitanzania ujuzi wa kuendesha mitambo mikubwa na kufanya shughuli za uchimbaji wa madini chini ya ardhi.

Amesema kampuni hiyo pia inashirikiana na Tume ya Madini na Wizara ya Madini katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuchagiza maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Kwa upande wa Tanzania, AUMS inatekeleza shughuli zake katika mgodi wa AngloGold Ashanti, huku kampuni mama ya Perenti ikiwa na shughuli za uchimbaji madini katika mataifa mbalimbali, ikiwamo Misri, Australia na Marekani.

Amesema kampuni hiyo inaendelea kutumia uzoefu na teknolojia kutoka katika masoko yaliyoendelea na kuleta ujuzi huo Tanzania, kwa lengo la kuongeza uwezo wa Watanzania na kampuni za ndani kushiriki zaidi katika sekta ya madini.