Breaking News

DKT. KIRUSWA AIPONGEZA EQUITY BANK KWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WADAU WA MADINI

GEITA - Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameipongeza Equity Bank Tanzania kwa kutoa huduma za kifedha kwa wachimbaji wadogo na wakubwa pamoja na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Kiruswa ametoa pongezi hizo leo, Septemba 27, 2026, baada ya kutembelea na kukagua mabanda ya washiriki katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.

Amesema jitihada za taasisi na kampuni katika kutoa mitaji, teknolojia na huduma mbalimbali kwa wadau wa madini ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Amewataka wadau hao kuendelea kubuni na kutumia mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuimarisha sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Akizungumza katika banda hilo Mkuu wa Idara ya Biashara, Wateja wa Kati, Wadogo na Binafsi wa Equity Bank Tanzania, Bi Theresia Mayanie, amesema benki hiyo inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mitambo, mtaji wa biashara na vifaa kwa wanaojihusisha na shughuli za kuongeza thamani ya madini.

Bi Mayanie amesema Equity Bank pia inatoa mikopo kwa wafanyakazi katika sekta ya madini na wadau mbalimbali wanaohusika katika mnyororo wa thamani, sambamba na kutoa elimu ya fedha kuhusu usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu na uwekezaji.

Maonesho hayo yameanza Septemba 23, 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 3, 2026, huku yakilenga kuwaunganisha wadau wa sekta ya madini na kuonesha teknolojia na fursa mbalimbali katika sekta hiyo.