MASAUNI: SAYANSI, TEKNOLOJIA MUHIMU KUKUZA UCHUMI WA BLUU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, amesema matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ni muhimu katika kuongeza mchango wa uchumi wa bluu na kuhakikisha rasilimali za bahari, maziwa, mito na maeneo ya pwani zinatumika kwa tija na uendelevu.
Masauni amesema hayo wakati akifungua rasmi Kongamano la Tano la Kimataifa la Sayansi na Uchumi wa Bluu, akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Deogratius Ndejim, ambaye alishindwa kuhudhuria kutokana na msiba wa mume wa Rais Samia Suluhu Hassan, marehemu Mzee wetu, na hivyo kuhitajika kushiriki katika shughuli za mazishi Zanzibar.
Amesema serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kuhakikisha rasilimali za majini zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, huku ikiimarisha tafiti, teknolojia na ubunifu katika sekta mbalimbali za uchumi wa bluu.
Kwa mujibu wa Masauni, uchumi wa bluu una fursa kubwa katika uvuvi na ufugaji wa samaki, utalii wa baharini, usafirishaji, biashara, nishati, pamoja na matumizi ya rasilimali za baharini katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.
Amesema Tanzania ina nafasi ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na bandari zake zinazohudumia Tanzania na nchi jirani, hivyo uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji ni muhimu kwa kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na muda wa usafirishaji na kuimarisha ushindani wa nchi.
Katika hatua hiyo, amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya reli, ikiwemo SGR, reli ya kati na TAZARA, sambamba na kuimarisha huduma za bandari ili kukamilisha mnyororo wa usafirishaji na kuchochea biashara ya ndani na kimataifa.
Amesema pia serikali inaendelea na ukarabati wa meli katika maziwa ya Tanganyika, Nyasa na Victoria, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kutengeneza meli na vyombo vya majini.
Masauni amesema hatua hizo zinaenda sambamba na ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu, akisisitiza umuhimu wa vyuo na taasisi za utafiti kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye katika uchumi wa bluu.
Ameongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera, mifumo ya usimamizi na ulinzi wa rasilimali za majini, kuongeza uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuharakisha matumizi ya teknolojia na kukuza rasilimali watu.
Aidha, amewataka sekta binafsi kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uchumi wa bluu, ikiwemo biashara ya kaboni ya baharini, teknolojia za baharini, kuongeza thamani ya mazao ya bahari na huduma za kidijitali.
Masauni amesema mafanikio ya uchumi wa bluu hayawezi kufikiwa na nchi moja pekee kwa kuwa bahari na rasilimali za majini zinaunganisha mataifa, hivyo ushirikiano katika tafiti, teknolojia, usimamizi wa rasilimali na uhifadhi wa mazingira ni muhimu.
Amepongeza Chuo cha Bahari dar es salaam DMI na wadau wengine kwa kuandaa kongamano hilo, akisema linatoa fursa kwa watafiti, watunga sera, sekta binafsi, taasisi za elimu, wabunifu na wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu namna bora ya kutumia sayansi na teknolojia kukuza uchumi wa bluu.
Ametangaza rasmi kufunguliwa kwa Kongamano la Tano la Kimataifa la Sayansi na Uchumi wa Bluu, akiwataka washiriki kutumia mkutano huo kutoa mawazo na mapendekezo yatakayotekelezeka kwa ajili ya maendeleo endelevu ya uchumi wa bluu nchini Tanzania na Afrika.







