NCCR-MAGEUZI YAKOSOA KAULI YA KIONGOZI WA DINI KUHUSU UCHAGUZI
DAR ES SALAAM: Chama cha NCCR-Mageuzi kimekemea na kueleza kusikitishwa na kauli ya kiongozi mmoja wa dini kuhusu ushiriki wa vyama vya siasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikisema matamshi hayo yanadhalilisha vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi huo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Idara ya Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi, Faustin Sungura, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Sungura amesema kiongozi huyo wa dini akichangia mada katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani yaliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Kwa mujibu wa Sungura, katika mjadala huo kiongozi huyo alisema baadhi ya vyama vya siasa vilikataa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku vingine vikishiriki kwa kuwa “wasindikizaji wa mchakato.”
Hata hivyo, Sungura amepinga kauli hiyo akisema si sahihi kusema vyama kadhaa vilisusia uchaguzi huo.
“Umma unajua hakuna vyama vilivyosusia uchaguzi, ni chama kimoja tu,” amesema Sungura.
Amesema NCCR-Mageuzi kimeona kauli hiyo kama udhalilishaji kwa vyama vya siasa vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kwamba ni muhimu kauli kuhusu mchakato wa uchaguzi zitolewe kwa usahihi.




