Breaking News

NECTA YATOA RATIBA MPYA YA MTIHANI YA TAIFA 2026

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Amer Hafidh, amesema Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) imefanya marekebisho ya ratiba ya mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, kwa lengo la kuhakikisha mitihani hiyo inaendeshwa kwa ufanisi na utulivu.

Akizungumza jijini DSM wakati akitoa taarifa ya kuhusu uendeshaji wa mitihani ya taifa kwa mwaka 2026 ,Wanu amesema marekebisho hayo yamezingatia pia utabiri wa uwepo wa mvua za El-Nino, ambapo upimaji wa Darasa la Pili, Darasa la Nne na Kidato cha Pili utafanyika mwezi Oktoba, huku Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne ikianza mwezi Oktoba na kukamilika mwanzoni mwa Novemba 2026. 
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania Profesa Said Ally Mohamed amesema mitihani ya darasa la nne inatarajiwa kuanza Tarehe 5 na 6 mwezi Oktoba, darasa la pili ni tarehe 7 na 8 mwezi Oktoba huku mitihani ya kidato cha pili ikifanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23 na kidato cha nne itaanza Oktoba 19 hadi Novemba 6 mwaka huu.

Aidha Profesa Mohamed amewataka wanafunzi, wazazi na walezi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Baraza la Mitihani Tanzania kuhusu ratiba ya masomo na maelekezo ya uendeshaji wa upimaji na mitihani ya Taifa kwa mwaka huu.