WIZARA YATAKA SHERIA RAFIKI KUCHOCHEA UCHUMI WA BULUU
DAR ES SALAAM. Wizara ya Katiba na Sheria imesema inaendelea kuhakikisha sheria zinazosimamia uchumi wa buluu zinafanyiwa maboresho ili kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji, huku ikihakikisha utajiri wa asili na maliasili za nchi unanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasili wa Wizara ya Katiba na Sheria, Neema Mwanga, wakati akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu.
Mwanga amesema wizara hiyo ina jukumu la kusimamia sera na sheria zinazohusiana na utajiri wa asili na maliasili, ikiwemo shughuli zinazofanyika katika bahari, maziwa na maeneo mengine yanayohusiana na uchumi wa buluu.
Amesema wizara inalenga kuweka mizania kati ya kuvutia uwekezaji na kulinda na kusimamia utajiri wa asili na maliasili za nchi ili kuhakikisha uwekezaji unaleta manufaa ya muda mrefu kwa Taifa.
“Tunapoangalia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, tunahakikisha sheria zote zinakuwa rafiki na wezeshi katika kusimamia masuala ya uchumi wa buluu,” amesema Mwanga.
Amesema baadhi ya sheria zinazoweza kuwa kikwazo katika kuvuna, kutumia na kuwekeza katika utajiri wa asili na maliasili zinaendelea kufanyiwa marekebisho ili kuendana na mahitaji ya sasa na kuwezesha uwekezaji zaidi katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Mwanga, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatambua nafasi kubwa ya sekta binafsi katika kukuza uchumi, hivyo mazingira ya kisheria yanapaswa kuwawezesha wawekezaji kushiriki kikamilifu katika sekta za uchumi wa buluu, ikiwemo uvuvi na shughuli nyingine zinazohusiana na rasilimali za majini.
“Tunataka mwekezaji anapofika nchini akute sheria ambazo ni rafiki na zitamwezesha kuwekeza katika uchumi wa buluu na kujenga maendeleo endelevu ya kiuchumi,” amesema.
Hata hivyo, amesema pamoja na kuvutia uwekezaji, wizara ina jukumu la kuhakikisha uwekezaji unaofanyika katika uchumi wa buluu unawanufaisha wananchi, huku wananchi wakishirikishwa na kupewa elimu kuhusu fursa zilizopo ili waweze kuzitumia kujiletea maendeleo.
Aidha, amesema Wizara ya Katiba na Sheria ina kitengo maalumu kinachoshughulikia utatuzi wa migogoro ya uwekezaji na biashara kwa kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka wizara hiyo, Daniel Baki, amesema kitengo hicho kinahamasisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro kati ya wawekezaji na wadau mbalimbali.
Amesema kitengo hicho pia kinahusika na usajili wa wataalamu wanaotoa huduma za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, wakiwemo wapatanishi na wawezeshaji wa majadiliano.
Baki amewataka watu wanaotaka kusajiliwa kutoa huduma hizo kutumia mfumo wa kielektroniki wa NARIS, ambao unapatikana kupitia kivinjari cha intaneti.
Amesema wananchi na wadau wanaohitaji maelezo zaidi kuhusu njia mbadala za utatuzi wa migogoro wanaweza kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika kongamano hilo.
Naye Richard, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, amesema sheria ni nyenzo muhimu katika kuweka mazingira yanayowezesha uwekezaji unaozingatia maslahi ya Taifa.
Amesema Tanzania inahitaji mfumo imara wa kisheria unaoweka mazingira wezeshi kwa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi, hususan katika sekta ya uchumi wa buluu, ili kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





