DC MPOGOLO AWAPA CHANGAMOTO VIJANA WA JOGGING: KIMBIENI AFYA, MKIMBILIE NA FURSA ZA KIUCHUMI
DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewahimiza vijana wanaoshiriki shughuli za jogging kuungana na viongozi wao ili kutumia fursa za kiuchumi, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Mpogolo alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa mbio za pole za City to City, zilizoandaliwa na Shirikisho la Jogging Ilala (IJA) chini ya kauli mbiu “Amani na AFCON Salama”, zilizoshirikisha washiriki zaidi ya 6,500 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa mbalimbali, ikiwemo Lindi, Mtwara, Morogoro na Dodoma.
Alisema jogging hazipaswi kuwa shughuli za mazoezi na burudani pekee, bali pia ziwe jukwaa la vijana kujadili fursa za maendeleo na namna ya kuboresha maisha yao kiuchumi.
Mpogolo alisisitiza kuwa viongozi wa halmashauri na wilaya wana wajibu wa kuwaunga mkono vijana na vilabu vyao, akiwataka kutumia mikutano yao kuibua mawazo ya biashara na kuangalia namna ya kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri.
Aliongeza kuwa kuwawezesha vijana kiuchumi ni muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kuboresha maisha na kuongeza kipato cha Watanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alisema halmashauri itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za michezo na kutumia mikusanyiko ya vijana kuwaelimisha kuhusu fursa zilizopo.
Mabelya alieleza kuwa halmashauri inaendelea na uratibu wa vikundi vya vijana ili kuwasaidia kupata taarifa sahihi kuhusu usajili wa vikundi na taratibu za kuomba mikopo ya asilimia 10.
Alisema mikusanyiko kama ya jogging ni fursa muhimu ya kuwaunganisha vijana, kuwafikia kwa urahisi na kuwawezesha kushiriki katika mipango ya maendeleo ya kiuchumi.
Mbio hizo zilianzia katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, zikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Charangwa Selemani.







