Breaking News

DODOMA KUITUMIA CHAMWINO KUENEZA KILIMO IKolojia HAI HALMASHAURI SABA


Na Mwandishi Wetu - MKOA wa Dodoma unatarajia kutumia Halmashauri ya Chamwino kama shamba darasa la kufundishia halmashauri nyingine saba za mkoa huo mbinu za kilimo ikolojia hai, ili mradi mpya unaotelezwa na Taasisi Kivuli ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM) na PELUM Tanzania uweze kuenea mkoa mzima.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Msaidizi - Mipango na Uratibu wa mkoa huo, Charles Mduma, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Kilimo Ikolojia Hai kwa ajili ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Kupanua Masoko na Kuhakikisha Usalama wa Chakula Tanzania.

Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri mbili nchini ambazo ni Arusha na Chamwino, ambapo matarajio ni kuwezesha wadau wote wa mnyororo wa kilimo ikilojoa hai wananufaika.

Mduma amesema mkoa umepokea mradi huo kwa mikono miwili na kuwataka maofisa ugani kushirikiana na TOAM na PELUM Tanzania, ili malengo yaweze kufikiwa.
Amesema mkoa utahakikisha Halmashauri ya Chamwino inatekeleza mradi kwa viwango vinavyokubalika ili kuwa shamba darasa kwa halmashauri nyingine.

"Tunaamini kwamba hizi wilaya mbili zitafanya vizuri ili hata halmashauri zingine zikitaka kuingia kwenye programu hii, zitachukua kesi stadi kutoka kwenye halmashauri hizi mbili," amesema.

Aliongeza kuwa Mkoa wa Dodoma una halmashauri nane, na baada ya Chamwino kutekeleza mradi huu, mkoa utatumia uzoefu huo kuambukiza halmashauri saba zilizobaki.

"Sisi kama Mkoa wa Dodoma tutatumia Chamwino kama shamba darasa ili kuambukiza halmashauri zetu saba ambazo zimebakia," amesema Mduma.

Mduma alitoa ushauri kwa waandaaji wa mradi huo kuwa baada ya utangazaji na utekelezaji wa awamu hii ya miaka miwili, waangalie namna ya kuupanua mradi ili halmashauri nyingine za Dodoma ziweze kuingia kwenye programu hiyo.

"Ushauri wangu ni kwamba baada ya utangazaji wa mradi huu, kama inawezekana katika baadhi ya maeneo, halmashauri zingine ziingie, na focus kubwa ikiwa ni Mkoa wa Dodoma ambao tuna halmashauri nane," alisema.
Katibu tawala huyo alisisitiza kuwa mradi huu sio tu utaongeza uzalishaji na masoko, bali pia utasaidia afya ya Watanzania kwa kupunguza matumizi ya kemikali hatari.

"Issue ya afya katika mazao yetu ni muhimu sana. Msukumo wa mradi huu utasaidia sana katika afya ya Watanzania, hasa wa Mkoa wa Dodoma, kwa sababu tunajua bado kuna kemikali nyingi wanazitumia ambazo baadaye zinakuwa na madhara kwa binadamu," alisema.

Amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ina sehemu ya Kilimo na Mifugo inayoshughulikia masuala ya kilimo ikolojia, na kwamba mkoa umejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ipasavyo.

Meneja wa Miradi wa TOAM, Sandra Haule, amesema mradi huo ni wa majaribio na ni mara ya kwanza kwa TOAM kufanya kazi na mfadhili huyo mpya.

Amesema mradi huo wa miaka miwili wenye thamani ya Dola za Kimarekani 200,000, unaolenga kusaidia wakulima wa kilimo ikolojia hai kupata soko la uhakika la mazao yao, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

"Huu ni mradi wetu mpya. Tumepata ufadhili wa mdau mpya wa maendeleo anayeitwa Climate Works kutoka Marekani. Ni mradi wa miaka miwili na wenye thamani ya Dola 200,000," amesema Haule.

Sandra amesema mradi huo unatekelezwa Halmashauri ya Arusha na Chamwino ambazo zimeangukia katika maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa kwenye Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai uliozinduliwa mwaka 2025.

"Mkakati wa Taifa ulikuwa na malengo 12, lakini wadau walikaa na kuweka vipaumbele sita na kuainisha maeneo matatu ya majaribio: Arusha, Kanda ya Kati ambayo Dodoma inaangukia, na Kanda ya Ziwa ambayo Mwanza inaangukia," alisema.
Aliongeza kuwa kwa vile mradi ni mdogo, walichagua wilaya ambazo tayari zina chachu ya utambuzi wa kilimo ikolojia hai.

"Tulichagua Wilaya ya Chamwino kwa sababu tumekuwa na mahusiano nayo kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 10. Kwa upande wa Arusha, tuna mdau wetu IDP ambaye ni kinara wa kupeperusha bendera ya kilimo hai kanda ya kaskazini. Tukasema tufanye kazi na vikundi vya IDP," amesema.

Amesema mradi huu ni tofauti na miradi mingine kwa sababu hauendi kumfundisha mkulima mbinu za kilimo ikolojia hai.

"Mradi huu unaenda kumsaidia mkulima kuanzia pale ameshamaaliza uzalishaji. Tunafanya kazi na vikundi ambavyo tayari vinafahamu kilimo ikolojia hai ni nini. Tunaenda kuanzia pale kwenye production point," amesema.

Amesema mradi utaangalia changamoto zinazomkabili mkulima katika kupata masoko, na kuangalia upanuzi wa masoko (market access) pamoja na kuunganisha mifumo ya masoko.

"Kwa hiyo mradi huu unalenga kuangalia upanuzi wa masoko ili mkulima aweze kuuza mazao yake kwa uhakika," alisisitiza.

Mradi huo unatarajiwa kuwa daraja kati ya mkulima na mnunuzi, huku ukihakikisha mazao ya kilimo ikolojia hai yanatambulika na kupata bei nzuri.