Breaking News

MASHABIKI WAHAKIKISHIWA USALAMA KUELEKEA MECHI YA SIMBA NA YANGA

DAR ES SALAAM – Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeimarisha ulinzi na usalama kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga utakaochezwa kesho, Oktoba 10, 2026, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Temeke, Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Faustine Mafwele, amesema jeshi hilo linatambua ukubwa wa mchezo huo unaozikutanisha timu hizo kongwe kutoka jijini Dar es Salaam.

Mafwele amesema ulinzi umeimarishwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo mashabiki, wapenzi wa soka na wadau wengine, kwa lengo la kuhakikisha mchezo huo unafanyika katika mazingira ya amani na usalama.

Amesisitiza mashabiki na wapenzi wa timu hizo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa ligi, pamoja na taratibu za mikusanyiko, na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na usalama.

Aidha, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limezitakia timu za Simba na Yanga mchezo mzuri, huku likiwataka mashabiki kushangilia timu zao kwa amani na kuzingatia usalama kabla, wakati na baada ya mchezo.