MFANYABIASHARA MZAVA NA WENZAKE WATATU KORTINI KWA KUJIPATIA TSH MILIONI 16 KWA UDANGANYIFU
Mfanyabiashara Joseph Mzava na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutumia utambulisho usio halali, ikiwemo kujipatia Sh milioni 16.
Wakisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha, Wakili Michael Sindai alidai kuwa washtakiwa hao, ambao ni Joseph Mzava, Venrand Meshack, Frank Kusenga na Edson Kamalamo, wanakibiliwa na mashtaka 31 ambayo walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Julai na Agosti 2025.
Aidha, Wakili Sindai alidai kuwa Mzava alitumia majina ya Salim Mhene, maarufu kama “Tryagain”, Salim Abdallah na Mwanaid Majaar kujipatia fedha kutoka kwa Hamis Pelle na Suleiman Suleiman kwa njia ya udanganyifu.
Alidai kuwa miongoni mwa njia zilizotumika ni kudai kuwa anakusanya michango kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha watoto yatima na kuandaa mkutano wa uwezeshaji wanawake.
Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 4, 2026, kwa ajili ya kutajwa, huku washtakiwa wakirudishwa mahabusu.





