NGOME YA VIJANA ACT YATAKA WATAALAMU WA BIOTEKNOLOJIA WATAMBULIWE RASMI NCHINI
Dar es salaam - Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, ameiomba Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati changamoto zinazowakabili wataalamu wa bioteknolojia nchini, akitaka watambuliwe rasmi na kuwekewa mfumo wa kitaaluma na kiutumishi.
Nondo amesema ni muhimu serikali kuhakikisha wataalamu hao wanatambuliwa, wanapewa leseni na kuundiwa bodi ya kitaaluma pamoja na muundo wa utumishi utakaowawezesha kutumia elimu na ujuzi wao katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Nondo amesema hatua hiyo itasaidia kutumia ipasavyo maarifa yanayozalishwa katika vyuo vya nchini na kuhakikisha wataalamu wa bioteknolojia wanapata nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwamo afya, kilimo, viwanda na mazingira.
Amesema Ngome ya Vijana Taifa ya ACT-Wazalendo imepanga kuandika barua yenye ushauri na mapendekezo kwa Ofisi ya Makamu wa Rais, huku ikiomba nafasi ya kukutana na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ili kueleza kwa kina changamoto hiyo na kuwasilisha mapendekezo ya namna ya kuipatia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Nondo, nakala ya barua hiyo pia itawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa suala hilo linahitaji maamuzi ya kisera na utaratibu wa serikali.
Amesema hatua hiyo inalenga kuishirikisha Ofisi ya Makamu wa Rais katika kutafuta suluhisho la changamoto ambayo, kwa maelezo yake, imeshindwa kutatuliwa kupitia Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya.
“Tunaiomba Ofisi ya Makamu wa Rais ilibebe swali hili kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais na kusaidia nchi yetu kutatua changamoto ya wanabioteknolojia wanaozalishwa nchini,” amesema Nondo.
Ameongeza kuwa utambuzi rasmi wa kada hiyo ni muhimu kwa usalama wa taifa, usalama wa bidhaa na ulinzi wa sekta ya afya, akisisitiza kuwa mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na uwepo wa mifumo inayowatambua na kuwawezesha wataalamu husika.
Nondo amesema kutokuwepo kwa utaratibu unaotambulika wa kitaaluma na kiutumishi kunaweza kuzuia matumizi ya ujuzi wa wataalamu hao katika kutatua changamoto za maendeleo, hivyo kuitaka serikali kulipa suala hilo kipaumbele.
Amesema Ngome ya Vijana Taifa ya ACT-Wazalendo inaamini kuwa kupitia mazungumzo na uwasilishaji wa mapendekezo kwa viongozi wa serikali, changamoto hiyo inaweza kupewa mwelekeo wa kisera utakaowezesha wataalamu wa bioteknolojia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi




