Breaking News

TANROADS YAIMARISHA MIUNDOMBINU KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ameeleza kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imejiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa kuanza Oktoba 2026, kwa kufanya ukaguzi wa barabara na madaraja, kusafisha mitaro na makalavati pamoja na kuimarisha kingo za barabara katika maeneo hatarishi.

Akizungumza kuhusu hatua za kukabiliana na mvua hizo, Mhe. Kadogosa amesema Wizara imeandaa mpango wa dharura unaojumuisha ukaguzi wa maeneo yenye historia ya kuathiriwa na mafuriko, matengenezo kinga na ununuzi wa vifaa vitakavyotumika kukabiliana na dharura ili kulinda miundombinu na kuhakikisha usalama wa wananchi.
Kadogosa ameeleza hayo leo Oktoba 13, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu hali ya barabara nchini na hatua zinazochukuliwa na TANROADS katika kuzilinda barabara.

Sambamba na hilo, Waziri Kadogosa amewasilisha taarifa ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara nchini kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27 kwa kamati hiyo.