DOHA DIALOGUE: SERIKALI YAWEKA MKAZO USALAMA WA WATANZANIA WANAOFANYA KAZI GHUBA
DAR ES SALAAM — Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, amesema Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi za Afrika na zile za Ghuba kuhakikisha usalama, ustawi na haki za wafanyakazi wanaohamia nchi za Ghuba kutafuta ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mkutano wa Doha Dialogue, Yunus amesema Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo unaowakutanisha wawakilishi kutoka nchi za Ghuba (GCC) na nchi mbalimbali za Afrika kujadili masuala ya uhamaji salama wa wafanyakazi.
Amesema mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa kwanza uliofanyika mwaka 2025 mjini Doha, Qatar, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi wanaohamia nchi za Ghuba.
“Hususan ni usalama na haki ya mfanyakazi, jambo la kwanza. Haki zake tangu anapotoka hapa, anaposafiri na anapofika kule,” amesema Yunus.
Kwa mujibu wa Yunus, serikali inalenga kuhakikisha taarifa muhimu za mfanyakazi zinapatikana kabla ya kuondoka nchini, ikiwemo mwajiri wake, aina ya kazi, mshahara na namna atakavyolipwa, ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza anapokuwa katika nchi ya ajira.
Amesema pia ni muhimu kuhakikisha mfanyakazi anapofika katika nchi anayokwenda anakuwa na taarifa sahihi za mahali anapopokelewa, huku masuala ya afya na ustawi wake yakizingatiwa.
Yunus amesema kwa miaka ya nyuma kumekuwa na malalamiko kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyakazi wanaokwenda nchi za Ghuba, jambo lililosababisha serikali za nchi husika kuanza kufanya majadiliano na kuweka mifumo bora ya usimamizi wa uhamaji wa wafanyakazi.
Ameongeza kuwa ingawa mawakala bado wanatumika katika mchakato wa kupeleka wafanyakazi nje ya nchi, serikali inataka kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kupitia mifumo salama, yenye uwazi na inayolinda haki za mfanyakazi.
Mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Ghuba katika kuhakikisha uhamaji wa wafanyakazi unakuwa salama, wenye tija na unaozingatia haki za binadamu na sheria za kazi.




