Breaking News

TMA YATANGAZA UWEZEKANO WA UWEPO WA KIMBUNGA SIKU NNE ZIJAZO

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetangaza uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi, karibu na Visiwa vya Ushelisheli, umbali wa takribani kilomita 1,600 kutoka Pwani ya Tanzania, ambao unatarajiwa kuimarika na kuwa Kimbunga ndani ya siku nne zijazo.

TMA imeeleza kuwa mgandamizo huo unaelekea katika Pwani ya Tanzania na unatarajiwa kuimarisha kiasi mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa Pwani na maeneo jirani, hususan kuanzia Oktoba 24, 2026.

Kutokana na hali hiyo, TMA imewashauri watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa sekta husika, huku mamlaka hiyo ikiendelea kufuatilia mwenendo wa mgandamizo huo na kutoa taarifa zaidi kadiri itakavyohitajika.