TTCL YAKABIDHI VIFAA VYA USAFI KWA WILAYA YA ILALA, YASHIRIKI ZOEZI LA KUFANYA USAFI
DAR ES SALAAM – Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekabidhi vifaa vya usafi kwa Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha usafi wa mazingira na kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa na mafuriko.
Vifaa hivyo ni pamoja na fagio, glovu, barakoa na magari ya taka, ambavyo vitatumika kuimarisha shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ameishukuru menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL kwa kuunga mkono juhudi za Serikali, akisema mchango huo una thamani kubwa katika kulinda afya za wananchi na kuhakikisha mazingira ya jiji la Dar es Salaam yanakuwa safi.
Mpogolo amesema thamani ya msaada huo haipaswi kupimwa kwa fedha zilizotumika kununua vifaa, bali kwa dhamira ya shirika hilo ya kusaidia kulinda afya za wananchi, kuzuia magonjwa na kupunguza hatari ya mafuriko yanayoweza kusababishwa na kuziba kwa mitaro na mifereji ya maji.
Amesema ushirikiano wa taasisi mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za usafi zinafanyika kwa ufanisi, hususan katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.
.Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masuala ya Miundombinu na Kiufundi wa TTCL, Mhandisi Cecil Francis, amesema shirika hilo limeamua kushiriki katika shughuli za usafi na kuchangia vifaa vinavyohitajika ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda mazingira.
Francis amesema ushiriki wa TTCL hautaishia katika zoezi hilo pekee, bali shirika litaendelea kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Ilala pamoja na wananchi katika kuboresha mazingira na kuhakikisha jamii inapata huduma bora za mawasiliano kwa gharama nafuu.
Ameongeza kuwa TTCL itaendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa huduma za mawasiliano, ikiwemo intaneti kupitia teknolojia ya nyuzi za mawasiliano (fiber), huku ikiunga mkono juhudi za maendeleo ya jamii
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amesema halmashauri inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala ya kuhakikisha usafi unafanyika kila siku katika kata zote 36, badala ya kusubiri siku maalumu za usafi.
Mabelya amesema shughuli hizo zinahusisha usafishaji wa mitaro, uzibuaji wa chemba, utunzaji wa kingo za mito na kuz00 kwa saa 24, hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali na viongozi wa wilaya.











