TTCL YAZINDUA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA YAJA NA KAULI MBIU ‘HATUA YA ZIADA’
DAR ES SALAAM — Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema huduma bora kwa mteja ni wajibu wa kila mfanyakazi, likisisitiza umuhimu wa kwenda “Hatua ya Ziada” (The Extra Mile) katika kutatua changamoto na kuboresha uzoefu wa wateja.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, uliofanyika katika TTCL Kijitonyama FTC Experience Center, ambapo viongozi wa shirika, wafanyakazi na wateja walishiriki katika kuangazia namna ya kuboresha huduma na uzoefu wa wateja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kanda ya Kaskazini, Anitha Moshi, alisema kila mfanyakazi wa TTCL ana mchango wa moja kwa moja katika kujenga uzoefu mzuri wa mteja.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “The Extra Mile”, inalenga kuwahamasisha wafanyakazi kuwa proactive, kutambua changamoto kabla ya mteja kulalamika, kutoa suluhisho la kudumu na kuchukulia malalamiko kama fursa ya kuboresha huduma.
Moshi alisema TTCL itaendelea kuimarisha mifumo ya kupokea na kufanyia kazi mrejesho wa wateja kwa haraka, kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto, kutumia teknolojia kurahisisha malipo na upatikanaji wa huduma, pamoja na kuwawezesha wafanyakazi kutoa huduma bora.
Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Kaskazini wa TTCL, Aron Msonga, alisema shirika limeendelea kuboresha uzoefu wa wateja kupitia huduma za kisasa, ikiwemo Fiber Mlango kwa Mlango, inayolenga kuwafikishia wateja huduma ya intaneti moja kwa moja majumbani.
Msonga alisema TTCL pia inalenga kuwaelimisha wateja kuhusu matumizi ya intaneti katika mifumo ya smart home, ikiwemo udhibiti wa taa, vifaa vya nyumbani, kamera za ulinzi, mapazia na vifaa vingine vinavyoweza kuunganishwa na intaneti.
Naye Meneja wa Huduma kwa Wateja wa TTCL, Diwani Mwamengo, alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja ni fursa ya kulishukuru shirika kwa wateja wake, kutambua mchango wa wafanyakazi na kuendelea kujenga utamaduni unaomweka mteja kuwa kitovu cha shughuli zote.
Mwamengo alisema huduma bora haiishii katika kumpokea na kumsikiliza mteja, bali inahusisha kuelewa mahitaji yake, kutoa huduma kwa wakati, kutatua changamoto kwa haraka na kuhakikisha anapata uzoefu mzuri kila anapokutana na TTCL.
Baadhi ya wateja walioshiriki katika uzinduzi huo, wakiwemo Doreen Kavishe na Godlove Mziray, walisema matumizi ya huduma za TTCL yamewasaidia kupunguza gharama za intaneti huku wakipata huduma yenye kasi na inayokidhi mahitaji yao.
Mziray, anayesimamia kampuni za Sahara Media, alisema matumizi ya huduma za TTCL yamekuwa “game changer” kwake kutokana na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za intaneti kwa familia na shughuli zake.
Aidha, alisifu kasi ya intaneti pamoja na mwitikio wa timu ya kiufundi ya TTCL, akisema wataalamu hao wamekuwa wakijitokeza kutatua changamoto za huduma hata nyakati za jioni na asubuhi.
Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 inalenga kuimarisha mahusiano kati ya TTCL na wateja wake, kusikiliza mrejesho, kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kujenga utamaduni wa kutoa huduma bora kwa wateja.









