Breaking News

TUZO YA UBORA KATIKA UTALII ENDELEVU NA USIMAMIZI WA UHIFADHI YAKUNA WADAU

Wadau wa Uhifadhi nchini wameendelea kuimwagia pongezi kwa hifadhi ya Ngorongoro kutokana na ushindi wa kishindo ilioupata wa kushinda tuzo ya kutukuka ya Ubora katika Utalii Endelevu na Usimamizi wa Uhifadh iliyopokelewa mwishoni mwa wiki jijini Accra, Ghana.

Salamu za pongezi za karibuni zimetolewa na Taasisi ya Uhifadhi na Urithi nchini yenye makao makuu yake jijini Dar essalaam ambapo katika taarifa iliyotolewa na Mtendaji mkuu wa taasisi Costantine Akitanda imeeleza kuwa ushindi wa Ngorongoro ni ushindi wa wadau wote wa Uhifadhi.

“Tuzo hii inathibitisha upya utambulisho wa kudumu wa Ngorongoro kama chimbuko lenye ushahidi kisayansi wa asili ya binadamu, ambapo hatua za kwanza za binadamu zilisikika, uhifadhi endelevu wa urithi wa utamaduni uliopo, mazingira, wanyamapori wakiwa katika mazingira yao ya asili na gunduzi mbalimbali zinaleta upekee kuwa Ngorongoro ni bustani ya Eden iliyotunzwa” imeeleza taarifa hiyo

Taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja na Ngorongoro kuwa sehemu ngumu katika usimamizi kutokana na mfumo wake wa matumizi mseto ya ardhi lakini mamlaka hiyo imeweza kujipambanua katika uhifadhi endelevu

Akizungumza mara baada ya kurejea kutoka Accra, Ghana kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Abdul-Razaq Badru alisema kuwa tuzo hiyo imetokana na ushirikiano wa wadau wote katika mnyororo wa Uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii na kuongeza kuwa wadau wote wana wajibu wa kulinda urithi wake wa kipekee wa asili na utamaduni, huku tukihakikisha kuwa uhifadhi huo unaleta thamani ya kudumu kwa watu, asili na vizazi vijavyo.