Breaking News

UBIA WA TFS NA UKEREWE WACHOCHEA UCHUMI NA AJIRA KUPITIA SHAMBA LA MITI RUBYA

MWANZA: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe wamekutana kupitia Kamati ya Ubia wa Usimamizi wa Shamba la Miti la Rubya lenye ukubwa wa hekta 1,056, kujadili maendeleo ya shamba hilo na kupokea taarifa ya utendaji kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026.

Kikao hicho kilichofanyika Oktoba 19, 2026, katika Ofisi za Kanda ya Ziwa jijini Mwanza, kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dkt. Zainabu Bungwa, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi.
Akifungua kikao hicho, Dkt. Bungwa alisema ubia huo ulioanzishwa mwaka 2015/2016 ni kielelezo cha namna ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa unavyoweza kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kuleta manufaa kwa pande husika pamoja na wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo, Goodluck Mtigandi, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, alisema shamba hilo limekuwa na mchango kwa halmashauri na jamii inayolizunguka kupitia mapato, ajira za moja kwa moja na upatikanaji wa mazao ya misitu.
Alisema uvunaji wa miti ya kupunguza msongamano (thinning) unaofanyika katika shamba hilo umechangia upatikanaji wa malighafi za misitu kwa ajili ya viwanda, huku wananchi wa vijiji vinavyolizunguka wakinufaika na shughuli zinazotekelezwa.

Naye Katibu wa Kamati hiyo, Mhifadhi wa Shamba, PCO Festo Chaula, alisema shamba hilo linaendelea kuimarisha fursa za utalii ikolojia, huku kukiwa na matarajio ya kutumia rasilimali nyingine za misitu, ikiwemo utomvu, kwa wakati utakaofaa.