Breaking News

TRA YAMREJESHEA OMMY DIMPOZ GARI BAADA YA KULIPA KODI

Dar Es Salaam - Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemkabidhi msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Omary Nyembo maarufu kama Ommy Dimpoz, gari lake lililokuwa limekamatwa kutokana na kukiuka taratibu za forodha, baada ya kulipa kodi ya ziada iliyobainika kutolipwa wakati wa uingizaji wa gari hilo nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam, yakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Paul John Walalaze, ambaye amesema gari hilo lilikamatwa baada ya kubainika kuwepo kwa taarifa zisizo sahihi katika nyaraka za forodha.

Walalaze amesema Nyembo ameshirikiana na TRA katika kufuatilia suala hilo na kukamilisha malipo ya tofauti ya kodi iliyopaswa kulipwa, hatua iliyowezesha kukamilika kwa taratibu za kurejeshewa gari lake pamoja na nyaraka zake.

Amesema ukiukwaji wa taratibu za forodha katika uingizaji wa magari nchini unahusisha baadhi ya wafanyabiashara kuingiza magari kwa njia ya usafirishaji wa kimataifa (International Transit), lakini badala ya kuyapeleka katika nchi husika, huyachepusha na kuyaacha nchini bila kukamilisha taratibu za kisheria.
Ameongeza kuwa wengine hutumia vibali vya muda vya uingizaji wa magari (Temporary Importation), vinavyoruhusu magari ya kigeni kutumika nchini kwa muda maalumu, lakini huyauza au kuyaacha nchini na kuyafanyia usajili wa ndani kinyume na masharti ya vibali hivyo.

Aidha, amesema kuna baadhi ya waingizaji wanaowasilisha taarifa zisizo sahihi kuhusu magari katika mfumo wa forodha wa TANCIS, ikiwemo kubadilisha taarifa za namba za chassis, modeli na mwaka wa kutengenezwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha kodi kinachopaswa kulipwa.

Kutokana na hali hiyo, Walalaze amewataka wamiliki wa magari yaliyoingizwa nchini kwa kukiuka taratibu hizo kutumia fursa ya msamaha uliotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, unaowaruhusu kujisalimisha na kulipa kodi inayostahili bila kulipa riba na adhabu, kabla ya Desemba 31, 2026.

Amesema magari 168 yalikuwa yamejitokeza katika kipindi cha Oktoba pekee, huku akibainisha kuwa baada ya muda wa msamaha kumalizika, TRA itaendelea na operesheni za kuyabaini na kuyakamata magari yote yatakayobainika kuingizwa nchini kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine, amewataka mawakala wa forodha kuhakikisha wanawasilisha taarifa sahihi za magari wanayosaidia kuyaingiza nchini, akionya kuwa wakala atakayebainika kuhusika na uwasilishaji wa taarifa za udanganyifu anaweza kufutiwa leseni pamoja na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.

Kwa upande wake, Ommy Dimpoz amesema ameamua kuweka wazi changamoto iliyomkabili ili kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa kufuatilia taratibu za kodi na forodha, akieleza kuwa awali aliamini gari lake lilikuwa limeingizwa nchini kwa kufuata sheria, lakini baadaye alibaini kuwepo kwa makosa katika taarifa za uingizaji zilizowasilishwa na msambazaji na wakala aliowatumia.

Amesema licha ya kuwa tayari alikuwa amelipa kodi, TRA ilimweleza kuwa kulikuwa na tofauti katika taarifa za gari hilo, hivyo alikubali kufuata maelekezo na kulipa kiasi cha kodi kilichobainika kuwa hakijalipwa.

Ommy Dimpoz amesema hakulazimishwa kuzungumzia suala hilo, bali ameamua kutumia nafasi yake kama mtu anayefuatiliwa na jamii kuhamasisha ulipaji kodi na kuwaonya Watanzania kuwa makini wanaponunua magari kutoka nje ya nchi.
Aidha, amewataka wamiliki wa magari wanaohisi kuwa na dosari katika taratibu zao za forodha kutumia fursa ya msamaha huo kabla ya Desemba 31, 2026, akisisitiza kuwa gharama za adhabu baada ya muda huo zinaweza kuwa kubwa zaidi kuliko kodi yenyewe.

Amesema atashirikiana na TRA kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya kodi, akibainisha kuwa kodi ni muhimu katika kugharamia huduma za umma na miradi ya maendeleo nchini.

Katika makabidhiano hayo, TRA imemkabidhi Ommy Dimpoz nyaraka za gari hilo zilizothibitisha kukamilika kwa malipo ya kodi pamoja na ufunguo wa gari, huku ikisisitiza kuwa magari yote yanapaswa kukidhi masharti ya forodha na usalama barabarani kabla ya kuanza kutumika.