Breaking News

WAZIRI MKUU AAGIZA MPANGO WA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TAASISI ZA DINI KATIKA ELIMU

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwelekeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kuandaa mpango wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika elimu, kwa kuzingatia uzoefu wa ushirikiano uliopo katika sekta ya afya.

Ametoa maelekezo hayo leo (Jumapili, Novemba 1, 2026), wakati akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya uzinduzi wa nyumba mpya ya ibada ya Bethel ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Nshara, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.

“Mheshimiwa Waziri, utaenda ukae na wenzako. Kaa na Waziri wa Afya,” amesema Dkt. Mwigulu
Dkt. Mwigulu ameelekeza wataalamu wa wizara hizo kuangalia namna ya kuimarisha ushirikiano katika elimu na kuandaa mpango utakaowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kupata ridhaa ya Serikali.

Maelekezo hayo yamefuatia maelezo kuhusu ujenzi wa kampasi ya Machame ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo), kinachomilikiwa na KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, pamoja na ombi la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa katika kutoa elimu.

Akifikisha salamu za Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya Taifa na itaendelea kushirikiana nazo katika kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema historia ya maendeleo ya Tanzania haiwezi kutenganishwa na mchango wa Kanisa, hususan katika elimu na afya, ambako taasisi za dini zimekuwa zikihudumia wananchi bila kujali imani zao.

“Hauwezi ukayataja maendeleo ya nchi yetu hii kwa ustadi wowote ule bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.

Dkt. Mwigulu amewapongeza washarika wa Nshara, viongozi wa Kanisa, kamati ya ujenzi na wadau wote waliofanikisha ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada, akisema wamefanya kazi kubwa inayostahili kupongezwa.