MUHIMBILI KUANZA KUTOA CHAKULA MWEZI UJAO KWA WAGONJWA WAOLAZWA
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Bw. Aminiel Aligaesha akizungumza na waandishi wa habari LEO
kuhusu hospitali hiyo kuanza kuboresha huduma ya chakula kwa wagonjwa
(special diet) wanaolazwa MNH kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Baadhi
ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini
wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo hicho LEO katika hospitali hiyo.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa MNH, Aligaesha akifafanua jambo
kwenye mkutano na waandishi wa habari LEO jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………….
Yawaondolea usumbufu ndugu wa wagonjwa kupeleka chakula mara tatu kwa siku
· Ndugu watapata muda wa kuendelea na shughuli za uzalishaji
Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) imeboresha huduma za chakula kwa wagonjwa wote watakaolazwa
kuanzia Julai Mosi, mwaka huu ili kuwaondolea ndugu wa wagonjwa usumbufu
na gharama za usafiri wakati wa wanapokwenda kuwaona ndugu zao
waliolazwa mara tatu kwa siku katika hospitali hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari leo Jijini Dar Es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya
Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha amesema
hospitali imeingia ubia na mzabuni ili kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa
wote wanaolazwa.
Bw. Aligaesha amesema Hospitali inataka kujikita katika majukumu yake ya msingi ambayo ni kushauri, kuchunguza na kutibu.
“Aidha Hospitali inataka
kuwaondelea adha ndugu wa wagonjwa ambao wamekuwa wakiingia gharama
kubwa hususani usafiri wa kuja Hospitalini mara tatu kwa siku, ambapo
kwa kukadiria gharama ya usafiri wa ndugu mmoja wa mgonjwa ni kati ya
shilingi 6,000/= na 10,000/= kwa siku, kulingana na mahali anapotokea
bila kujumuisha gharama za kuandaa chakula cha mgonjwa ambacho mara
nyingi ni chakula maalumu. Na kama mgonjwa akilazwa zaidi ya siku tano
hadi 10 ndugu mmoja wa mgonjwa gharama atalipia fedha nyingi kwenye
usafiri” amesema Bw. Aligaesha
Ameongeza kuwa adha ya pili
wanayopata ndugu ni usumbufu ambapo inabidi kuacha shughuli nyingine za
uzalishaji ili kuja kuleta chakula mara tatu kwa siku, hivyo
kuingiliana na shughuli zao za kiuchumi na kimandeleo na kushindwa
kuzalisha. Hivyo jukumu hili linachukuliwa na Hospitali kuwaondolea adha
hii.
·
“Pia kuna baadhi ya ndugu
wamekuwa wakishindwa kuwaletea chakula wagonjwa wao hivyo hospitali
ililazimika kuwapatia chakula ambacho kilikuwa kwa ajili ya wagonjwa
wanaotoka mikoani wasio na ndugu hapa Dar Es Salaam” amesisitiza Bw.
Aligaesha.
Amesema kumekuwepo na
ongezeko la msongamano wa watu ndani ya Hospitali toka asubuhi saa 12
mpaka saa 12 jioni, suala linaloingiliana na utoaji huduma hasa saa za
mchana kwani muda wa saa 6.00 hadi saa 8.00 mchana ulikuwa unaingiliana
na majukumu ya kiutendaji ambapo majopo mbalimbali ya watalaamu yamekuwa
yakiendelea na raundi za wagonjwa waliolazwa. Hii wakati mwingine
imesababisha mgonjwa kutokupata huduma stahiki kutokana na muingiliano
huu.
·
“Vile vile msongamano huu ni
changamoto kwa ajili ya masuala ya kiusalama ambapo kati ya watu
wanaoingia Hospitali kwa kigezo cha kuja kuona wagonjwa kuna wanaoingia
kwa lengo la kufanya uhalifu ikiwemo wizi wa mali za Hospitali, magari
pamoja na vifaa vya magari” alisisitiza.
Amesema kwa kufanya hivyo,
Hospitali itapunguza baadhi ya gharama za uagizaji wa vyakula kwa
wazabuni, kulinda upotevu na baadhi ya vyakula kuharibika wakati
mwingine kwani utunzaji wa vyakula una mahitaji makubwa.
Bw. Aligaesha amesema
Hospitali inakusudia kutoa chakula chenye ubora na viwango vinavyotakiwa
kwa wagonjwa ikiwemo kutoa chakula maalumu (special diet) kwa wagonjwa wenye uhitaji huo.
Kuhusu utaratibu huo Bw.
Aligaesha amesema Mzabuni ndiye atakayepika chakula kwa wagonjwa wote
waliolazwa na atatayarisha, atakipeleka na kukikabidhi katika wodi
husika ambapo jukumu la kumpa mgonjwa kifungua kinywa, chakula cha
mchana na jioni linabaki wa Hospitali.
Amesema wagonjwa watapatiwa
milo mitatu kwa siku yaani asubuhi, mchana na jioni kazi itakayofanywa
na muuguzi wa zamu ambaye atahakikisha wagonjwa wote wamepata chakula
kufuatana na mahitaji (diet list) iliyowasilishwa jikoni kutokana na mahitaji yao ya kiafya.
Kutokana na uamuzi huu,
utaratibu wa ndugu kuleta chakula kwa wagonjwa waliolazwa wakati wa
mchana umefutwa na hivyo mchana hatutakuwa na nafasi ya ndugu kuja
kutembelea wagonjwa. Muda wa kutembelea wagonjwa utakuwa asubuhi saa 12
hadi saa moja kamili na saa 10:00 jioni hadi saa 12:00jioni ndipo ndugu
wataruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zao waliolazwa. Katika muda huo
ndugu ataruhusiwa kuja na chakula chochote anachofikiri atamuongezea
mgonjwa wake kama matunda n.k
Bw. Aligaesha amesema mgonjwa
aliyelazwa atachangia kiasi cha shilingi 50,000 atakapolazwa ambapo
kati ya hizo, shilingi elfu 10,000 itakuwa ni gharama ya kumuona daktari
(Consultation), shilingi elfu 10,000 ikiwa ni gharama ya kulazwa
na bei ya chakula itakuwa shilingi elfu 30,000 sawa na shilingi elfu
6,000 kwa siku. Wastani wa mgonjwa kukaa wodini ni siku tano. Gharama
hizo zinahusika kwa muda wote atakaokuwa amelazwa.
Kwa sasa Hospitali inatoa
chakula kwa wagonjwa 650 ambao wamepata rufaa kutoka hospitali za nje ya
mkoa wa Dar es Salaam kwa gharama wastani wa shilingi 1.8 bilioni kwa
mwaka, sawa na shilingi 150 milioni kwa mwezi kwa vyakula pamoja na
gharama nyingine kama vile za nishati. Takribani wagonjwa kati ya 600
na 700 ambao rufaa zao ni kutoka Hospitali za Dar es Salaam walikuwa
hawapati chakula kutoka Hospitalini, na ilibidi ndugu zao wawaletee
chakula. Hata hivyo, Hospitali ilikuwa inawapatia chakula tu kama ndugu
zao wakishindwa kufanya hivyo.
“Uongozi wa Hospitali unaamini
kwamba mabadiliko haya hayatamuongezea mgonjwa gharama, bali
yatampunguzia gharama pamoja na ile adha kama ilivyoainishwa hapo juu.
Aidha, uongozi unaamini kwamba uamuzi huu unaendana na azma nzima ya
kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuboresha
mazingira ya Hospitali. Tunaomba ushirikiano wenu katika kutekeleza
jukumu hili ili kusudi wagonjwa waweze kuhudumiwa vizuri zaidi”
amesisitiza Bw. Aligaesha.



